SMZ yafunga mkaja kudhibiti unyanyasaji wanawake na watoto Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema  kutokana na kuongezeka  kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji  dhidi ya wanawake na watoto hapa Zanzibar inakusudia  kuzindua  mpango kazi wa kitaifa  wa kumaliza kadhia hiyo inayowakabili wanajamii.


Waziri wa kazi,Uwezeshaji,Wazee,Vijana,Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico pamoja na Wawakilishi mbalimbali wa mashirika ya kimataifa wakisikiliza maswali yanayoulizwa na Waanishi wa Hababari kuhusu uzinduzi wa vitendo vya ukatili  na udhalilishaji wanawake na watoto Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya uzinduzi wa mpango huo unaotarajiwa kuzinduliwa kesho katika hoteli ya Zanzibar beach resort Mjini Zanzibar Waziri wa kazi,Uwezeshaji,Wazee,Vijana,Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico amesema mpango unalenga  kutoa mwongozo kwa namna  ya kumaliza  masuala ya ukatili na udhalilishaji  kwa wanawake na watoto visiwani Zanzibar.

Amesema bado wanawake na watoto wanafanyiwa vitendo vya udhalilishaji siku hadi siku jambo linalopelekea  athari kubwa katika kijamii,kiafya na hata kiuchumi kwa waathirika wa vitendo hivyo.

Castico amesema licha ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa  katika kukabiliana na vitendo hivyo lakini bado  kuna changamoto nyingi zinazorudisha nyuma jitihada ikiwemo uwajibikaji mdogo kwa baadhi ya watendaji wa masuala ya udhalilishaji,jamii yenyewe kuwaonea muhali watenda udhalilishaji.

Amesema pia mpango huo utaendeleza kampeni ya kuelimisha  umma na kuhamasisha jamii kushughulikia masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto iliyozinduliwa mwaka 2014  na Rais wa Zanzibar Dr.Ali Mohamed Shein.

Hata hivyo Castico amesema  lengo la Serikali kwa kushirikiana na asasi za kiraia,mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo ni kuhakikisha wanavitokomeza vitendo vya aina zote za udhalilishaji pamoja na kuwachukulia  hatua watenda  maovu  kwa wanawake na watoto hapa nchini.

Kwaupande wao Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kutoka Save the Children,UNICEF,UNFPA pamoja na UN WOMEN wamesema kupitia mpango huo unaotarajiwa  kuzinduliwa Zanzibar utasaidia kuondoa kabisa aina zote za ukatili  na udhalilishaji na kuweza kuwapatia heshima wanawake na watoto.

Wamesema wataongeza ushirikiano kwa serikali na kuunga mkono  mapambano  ya ukatili na udhalilisahji ili  kumaliza kabisa kadhia hiyo inayorudisha nyuma maendeleo na kudumaza uchumi wa nchi.

Aidha wamesema mpango huo utaibua mbinu mbadala za  kukabiliana na udhalilishaji endapo jamii ya wazanzibar itatumia busara na kufanya kazi kwa mashirikiano.

Zaidi ya Shilling Billion 44 zimepangwa kutumika katika utekelezaji wa mpango huo hapa zanziabr.
chanzo:Zanzibar24

Comments