SMZ kuwatunuku vyeti Mafundi bingwa wasiokuwa na vyeti.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Mamlaka ya Mafunzo ya Amali, inaandaa utaratibu wa kuwatambua rasmi mafundi bingwa wa kazi mbalimbali wasiokuwa na vyeti vya chuo vinavyotambulisha ujuzi wao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Bakari Ali Silima, alisema kuna wajuzi wengi wa kazi za mikono na ufundi mitaani, ambao hawakubahatika kwenda vyuoni lakini wanafanya kazi nzuri.
Alisema mafundi wengi wa fani mbalimbali hawajenda vyuoni ambako baada ya kuhitimu wanafunzi hutunukiwa vyeti na kuwarahisishia kupata ajira katika taasisi na kampuni zinazowahitaji.
Silima alitoa mfano wa mafundi wa ujenzi wa nyumba, wachongaji majahazi, wahunzi, washoni na fani nyengine ambao taaluma zao wamezipata kupitia mafundi wengine au kurithi kwa wazazi au walezi wao.
Hata hivyo, alisema pamoja na ujuzi walionao, inakuwa shida kwao kukubaliwa katika ajira za kampuni hasa za ujenzi wa majengo na miundombinu zinazopatikana kutokana na miradi inayotekelezwa nchini.
Alisema ingawa wengi wa wajuzi kama hao hujiajiri wenyewe, lakini pia kunapojitokeza ajira za msimu zitokanazo na miradi inayohitaji wataalamu, wanakwama kwa kukosa vyeti vinavyotambulisha taaluma zao.
“Ni kweli tuna mafundi wengi mitaani ambao husoma kwa mabingwa mpaka wanajua kazi. Kwa mfano mtu anakwenda kujikabidhi yeye mwenyewe kwa fundi wa majahazi, anafundishwa mpaka anahitimu lakini anakosa sifa ya kuwa na cheti,” alisema Mkurugenzi huyo.
Alisema kutokana na umuhimu wake, Mamlaka ya Mafunzo ya Amali inachukulia mfumo wa kuchota ujuzi kutoka kwa mafundi wakongwe ni sehemu ya mafunzo ya kazi, na kwamba iko katika maandalizi ya kuandaa utaratibu wa kuwatambua rasmi mafundi kama hao.
Silima alisema tayari Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Tanzania Bara (VETA) inayo programu hiyo inayofanyika kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za kimataifa, na kwamba mamlaka yake imeshatembelea huko kwa ajili ya kuona namna ya kuitekeleza pia visiwani humu.
“Ni matumaini yangu kwamba katika muda mfupi ujao nasi tutaweza kufikia kama walivyo wenzetu wa VETA, pia tutashirikiana na wenzetu tafauti ili kuona jinsi gani tutaweza kuwafanyia mitihani wafanyakazi hao na kuwatathmini.
Hata hivyo, alieleza kuwa mpango huo utahitaji gharama kwa ajili ya kuwatafuta wataalamu husika wa kuwafanyia mafundi hao mitihani ya nadharia na vitendo ili kupima kiwango cha ujuzi wao.
Alisema baada ya kufanyiwa mitihani hiyo na kujiridhisha, mamlaka yake itawatunuku vyeti vya kutambua rasmi taaluma zao vitakavyowasaidia kukubalika katika soko la ajira za ufundi ndani na nje ya nchi.
 chanzo:zanzibar24.

Comments