Rais
John Magufuli ameziagiza wizara za Fedha na Mipango na Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa Tamisemi kuandaa mapendekezo na kupeleka bungeni
mwaka huu marekebisho ya sheria yanayotaka kulipwa kwa Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT) kwa miradi inayopata ufadhili kutoka kwa wadau wa
maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia.
Alitoa
agizo hilo juzi wakati akihutubia wananchi wa Korogwe waliohudhuria
ufunguzi wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi iliyogharibu Sh bilioni nne
eneo la Kilole. Dk Magufuli alisema utaratibu huo unafanya serikali
kulipa VAT kwa serikali yenyewe jambo ambalo si sahihi kwa kuwa fedha
hizo zingetumika kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Alitoa
agizo hilo baada ya Naibu Waziri Tamisemi, Selemani Jaffo kueleza kuwa
ipo changamoto ya kisheria inayokabili miradi ya maendeleo
inayotekelezwa na serikali kutakiwa kulipa VAT na kusababisha serikali
kulipa fedha za ziada Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa sababu mikopo na
ruzuku kutoka kwa wafadhili hazitengi malipo ya kodi.
“Nawaagiza
mawaziri wa wizara zote mbili kuandaa marekebisho ya sheria hii ambayo
ilipitishwa mwaka 2015 ili mwezi Septemba iweze kurekebishwa bungeni...
tunahitaji fedha, lakini sio kwa kila kitu tutozwe VAT hiyo ni
kujichelewesha hayo mambo ni ya ovyo lazima tuyaache,” alieleza Dk Magufuli.
Awali,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),
January Makamba alimuomba rais kushughulikia mgogoro wa kiwanda cha
kusindika chai cha Mponde wilayani Lushoto ambao umechukua muda mrefu na
kusababisha wakulima wa Jimbo la Bumbuli wilayani humo kushindwa
kujiendeleza kiuchumi.
Stendi
iliyojengwa mjini Korogwe ni miongoni mwa mradi 11 inayojengwa na
kusimamiwa na Tamisemi kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika baadhi ya
halmashauri nchini.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments