Mwanamke auwawa kwa kukatwa shingo.

Picha haihusiana na tukio husika.
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma, linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za mauaji ya mwanamke mmoja mkazi wa Kigoma aliyeuwawa kwa kuchinjwa na kisha kichwa chake na baadhi ya viungo vyake kuchomwa moto katika Kitongoji cha Chang'ombe Kijiji cha Chamwino. 


Kamanda wa Polisi kutoka makao makuu ya nchi Dodoma, Lazaro Mambosasa amemtaja mwanamke huyo kuwa ni Mariam Saidi na kusema tukio hilo  limetokea usiku wa kuamkia leo saa 10:00
 alfajiri katika kitongoji cha Chang’ombe kijijini hapo na mwili wa marehemu kukutwa nyumbani kwa mganga wa kienyeji aliyetambuliwa kwa jina la Ashura Mkasanga Mratha huku sura ya marehemu ikishindwa kutambulika baada ya kichwa chake kuchomwa moto.

Kamanda Mambosasa amesema mganga huyo wa jadi asiye na kibali cha kuendesha shughuli za tiba asili pia amekutwa akilaza wagonjwa nyumbani kwake na kufanya matambiko pamoja na kupiga ramli chonganishi ambayo ni kinyume na sheria.

Pamoja na hayo, Mganga huyo amekutwa akiwafanyia tohara  watoto.

Kwa upande mwingine, Kamanda Mambosasa amesema amewakamata wagonjwa nane waliyokuwa wamelazwa pamoja na mume wa mganga huyo ambaye ametambulika kwa jina la Noel Mazengo  na wasaidizi wake kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
chanzo: eatv.

Comments