Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe amemtaka Rais John Magufuli kuacha kuwafunga
mdomo Watanzania na kuijenga Tanzania kuwa Taifa la hofu.
Akihutubia
mkutano wa hadhara katika mji wa Bomang’ombe jana, kwa takribani dakika
30, Mbowe alisema hata kama Rais atawazuia Watanzania milioni 53
kusema, basi mawe yatasema.
Mbowe
ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alienda mbali na
kusema Chadema imejipanga kuwafungulia kesi wakuu wa wilaya wote
waliowaweka ndani viongozi kwa saa 48 katika maeneo yao.
Alisema
katika hali ya kutatanisha Rais Magufuli aliyeapa kuilinda Katiba ya
nchi amegeuka na kuzuia mikutano ya hadhara ambayo ipo kisheria.
“Siasa
katika nchi yetu inaongozwa na Katiba na sheria ya vyama vya siasa ya
mwaka 1992, lakini katika mazingira ya kutatanisha kabisa Rais amezuia
mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020,” alisema na kuongeza:
“Rais
usiwazuie watu wako kusema, ukiwazuia mawe yatasema. Kama kuna kitu
kibaya duniani ni kuvunja Katiba ya nchi, nataka nimwambie huwezi
kufunga midomo ya watu milioni 53.”
“Tunajenga
nchi ya watu waoga. Rais anataka aonekane ni mbabe, bungeni
tunadhibitiwa hadi hotuba zetu lazima zipitiwe na watu wa usalama waseme
uondoe hiki. Watu wenye dhambi ndio waoga.”
Mbowe,
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Hai alisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere aliwahi kusema mara nyingi kuhusu umuhimu wa viongozi
kuheshimu Katiba na akataka iwe mwiko kwa kiongozi kuidharau.
Akizungumzia
kamatakamata ya viongozi, alisema hali hiyo ndio inaimarisha zaidi
upinzani kuliko wakati wowote ule na kusema watawaburuza kortini wakuu
wa wilaya waliokiuka sheria.
Mbowe
alisema baadhi ya wakuu wa wilaya wanatumia vibaya sheria ya kuwaweka
watu rumande kwa saa 48 akisema wengine wanaitumia kuwakomoa wale
wanaotofautiana nao kimtazamo.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisema hata wale
waliokuwa wanashangilia wimbo wa kuisoma namba nao wanaisoma namba hiyo
kwa Kiarabu na Kirumi.
“Huu
ni wakati wa kupambana zaidi. Wanatutia hofu kwa kutukamata ili
tusiseme, lakini nataka kusema saa ya ukombozi ni sasa. Tutaendelea
kusema kwa vile ni haki yetu,” alisema,
Meya
wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema Chadema ni chama cha siasa na
wanapambana na CCM ambayo hawajui kama ni chama kwa vile wakuu wa mikoa
na wilaya ndio wamegeuka viongozi wa CCM.
“Yaani
wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ndio wamegeuka viongozi wa CCM. Huko
nyuma Chadema tukisema tulikuwa tunajibiwa na Kinana (Abdulrahman) au
Nape (Nnauye),” alisema.
Kinana ni katibu mkuu wa CCM wakati Nape alikuwa katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho. Kwa sasa ni mbunge wa Mtama.
“CCM
iko wapi? Wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa ndio wanabeba ilani ya CCM.
Wananchi Hai msiogope. Chadema chini ya Mbowe haitatetereka kamwe,”
alisisitiza Meya huyo, ambaye pia amewahi kukamatwa.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments