OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
amesema kuwa kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya kimaendeleo baada ya
kuundwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya ndege vya Zanzibar kumeweza kuongeza
mapato na kuahidi kuimarika zaidi hali hiyo ndani ya kipindi chake cha
uongozi.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya
Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege pamoja na Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka hiyo kwa kufanya
mabadiliko makubwa katika viwanja vya ndege vya Zanzibar hatua ambayo
imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato katika viwanja
hivyo.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa licha ya baadhi ya
changamoto zilizopo lakini Mamlaka imeweza kupata mafanikio makubwa na
hivi leo viwanja vya ndege Unguja na Pemba viweza kuimarika na kuleta
tija kwa kuongeza mapato.
Akizungumza suala zima la fidia kwa wananchi waliojenga pembezoni mwa
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar Dk. Shein
alisema kuwa ni vyema likatafutiwa ufumbuzi kwa kuwatafuta wahusika na
kuwasikiliza madai yao ili hatua za malipo ziendele kuchukuliwa.
Akizungumza na uongozi wa Wizara hiyo kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya
Shirika la Nyumba pamoja na Uongozi wa Shirika hilo, Dk. Shein
alisisitiza haja ya Shirika hilo kuzitambua na kuziorodhesha ili kujua
idadi ya nyumba zao zote za Unguja na Pemba pamoja na zile za Wakala
hatua ambayo pia, itasaidia kuepusha udanganyifu.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Bodi ya Shirika hilo
pamoja na uongozi wa Shirika hilo kwa mafanikio makubwa yaliopatikana
kwa kipindi kifupi.
Alieleza haja ya kuwepo utaratibu wa kuwatambua wakaazi wananoishi
katika nyumba zote za Mji Mkongwe wa Zanzibar ili iwe rahisi katika
kutekeleza mipango ya Serikali huku akieleza azma ya Serikali ya kujenga
miji ya kisasa sambamba na kutekeleza mradi wa kufukia bahari katika
eneo la pwani ya Gulioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kisasa
zikiwemo hoteli.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa
Wizara hiyo walioongozana na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uhifadhi
na Uendelezaji Mji Mkongwe na Uongozi wa Mamlaka ya Uhifadhi na
Uendelezaji Mji Mkongwe na kueleza umuhimu wa kuweka utaratibu maalum
juu ya kupunguza foleni ya gari katika barabara inayopita katika
Bandari ya Malindi.
Aidha, alieleza haja ya kuzingatia na kufuata kanuni na misingi ya
Sheria iliyounda Bodi hiyo ili Mamlaka hiyo na Bodi yake iweze kufanya
kazi kwa ufanisi pamoja na kufuata Sheria nyengine zote muhimu huku
akieleza umuhimu wa uhifadhi wa mji huo.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alieleza
kwamaba tabia ya kukodishwa nyumba kwa kutumia vilemba ambapo hatua hiyo
ndio chanzo kikubwa cha upotevu wa nyumba za Serikali huku
akisikitishwa na baadhi ya wananchi waliopewa nyumba na Serikali na wao
kuzikodisha ama kuziuza bila ya kufuata taratibu na sheria zilizopo.
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali
Karume kwa upande wake alieleza hatua zzinazoendelea kuchukuliwa katika
Wizara yake katika kutoa ushirikiano uliopo kwa viongozi, wafanyakazi,
Bodi pamoja na wajumbe wake.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Abdulhamid
Yahya Mzee kwa uonde wake alisisitiza haja ya kuimarisha usalama katika
viwanja vya ndege vya Zanzibar kwani Mashirika ya ndege na hata wageni
hilo wamekuwa wakilipa kipaumbele.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Abdulhani Msoma
aalieleza kuwa mapato yanayokusanywa katika viwanja vya ndege
yameongezeka kutoka TZS Bilioni 12.9 mwaka 2011/2012 hadi kufikia TZS
Bilioni 39.3 mwaka 2016/2017.
Alieleza kuwa idadi ya mashirika ya ndege imeongezeka kutoka
mashirika 63 mwaka 2011 hadi mashirika 78 mwaka 2016 ambapo kati ya
mashirika hayo, mashirika ya kimataifa yameongezeka kutoka 39 mwaka 2011
hadi 48 mwaka 2016 na mashirika 24 ya ndani yameongezeka hadi kufikia
30 mwaka 2016.
Aliongeza kuwa idadi ya abiria imeongezeka kutoka 753,971 mwaka 2011
hadi abiria 1,032,043 mwaka 2016 sawa na asilimia 137 kati ya abiria hao
abiria wa kimataifa wameongezka hadi kufikia 529,696 mwaka 2016 kutoka
abiria 283,755 mwaka 2011.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar Mohamed Hafidh Rajab
alisema kuwa licha ya uchanga wa Shirika hilo lakini ukusanyaji wa
mapato yataongezeka kutoka TZS bilioni 1.6 mwaka 2017/2018 hadi kufikia
TZS bilioni 48 katika mwaka 2021/2022 huku akieleza azma ya ujenzi wa
nyumba za makaazi zikiwemo za wananchi wenye kipato cha chini.
Nao uongozi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe na Bodi
yake ulieleza kuwa baadhi ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na
washirika wa maendeleo wameonesha azma ya kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuuimarisha Mji Mkongwe wake ikiwa ni pamoja na
kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba huku ukieleza hatua
zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi yake.
Katika vikao vya leo, Dk. Shein alikutana na Uongizi wa Wizara hiyo
pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, uongozi
wa Mamlaka pamoja na Bodi ya Shirika la Nyumba na Bodi ya Wakurugenzi ya
Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe na uongozi wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
CHANZO: zanzibar24.
Comments