“Kukaa ofisini kuangaliana sura hakuwasaidii ushuhuda wa kile kilichofanyika kwa wananchi”Dkt. Shein.

Dk Shein, ameeleza hayo ukumbi wa chuo cha SUZA Mchanga mdogo wilaya
ya Wete kisiwani Pemba, wakati akuzungumza na wanachi, viongozi wa chama
na serikali, mara baada ya kupokea taarifa ya kikazi ya Mkoa wa
kaskazini Pemba.
Alisema, huu sio wakati tena wa kuganda ofisini ni lazima kazi
kuziacha kwa muda, na kwenda kwa wananchi waliomchagua, ili kuangalia
kile alichokiahidi juu ya utekelezaji wake.
Alisema kukaa ofisini kwa muda mrefu, hakuwasaidii wananchi na wala
hakuna ushuhuda wa kile kilichofanyika, hivyo ni lazima kuwatembelea.
Alieleza kuwa, ndio maana kwenye ripoti hiyo ya Mkoa, hataki kusema
chochote, hadi hapo atakapoisoma na kutembelea maeneo husika, kuona
utekelezaji wake.
“ Mimi nimeshaipokea ripoti, na kwa vile nipo Pemba mwenyewe
ntakwenda kuona haya yaliomo kwenye taarifa, maana sasa lazima sisi
viongozi tuhame ofisini na twende moja kwa moja kwa wananchi
kujiridhisha ”,alifafanua.
Akizungumzia kuhusu ripoti hiyo, rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, aliupongeza mkoa huo kwa taarifa nzuri na
ilioshiba.
Alisema ijapokuwa hajaisoma yote ripoti hiyo, lakini kutokana na
uwasilishwaji wake na alivyopokea taarifa, imeandaliwa vya kutosha na
inautekelezaji ndani yake.
“Taarifa yenu ya kikazi kwa kweli imeshiba na imebeba utendaji wa
kazi wa kila idara, lakini leo siseme kitu hadi nikimaliza ziara yangu,
nasubiri kwenye majumuisho ntasema na kuuliza”,alisema Dk Shein.
Katika hatua nyengine, rais huyo wa Zanzibar, amewapongeza wananchi,
viongozi wa chama na serikali kwa kuhudhuria kwenye uwasilishaji wa
taarifa hiyo, na kusema hapo ndio watapata taarifa sahihi.
“Mimi nashangaa kuona baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu na viongozi
wengine hawashiriki ziara kama hizi ambazo ni za kiutendaji, na wala sio
za kujifurahisha”,alifafanua.
Aliongeza kuwa, yeye baada ya kuchaguliwa na wananchi aliamua
kuwachagua wasaidizi wake, sio kwa kujuana wala kuangalia sura bali, ni
kwa kumsaidia hivyo kama kwenye ziara hiyo hawashiriki anashindwa
kuwafahamu.
“Kiongozi wa chama kwenye utekelezaji wa Ilani hii ya CCM ya mwaka
2015/2020 ananafasi yake na halikadhalika sisi viongozi wa serikali kama
mawaziri tunawajibu wetu mkubwa, lazima tuwepo”,alifafanua.
Akiwasilisha taarifa hiyo ya kikazi, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba
Mhe: Omar Khamis Othaman alisema maendeleo makubwa yameshapatikana ndani
ya Mkoa huo, ikiwa ni pamoja na maji safi na salama.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa, alimueleza rais huyo wa Zanzibar kuwa,
changamoto kubwa inayowakabili katika kuzimaliza kesi za udhalilishaji
ni wananchi kutokuwa tayari kutoa ushahidi mahakani.
“Tumefanikuwa kuunda kamati za mkoa na wilaya juu ya kupinga
udhalilishaji, lakini sasa wananchi bado baadhi yao wamekuwa wasugu
kushirikiana na vyombo vya kisheria”,alilalmikia.
Aidha alifafanua kuwa, ushirikiano mkubwa uliopo baina ya wananchi na
kamati ya ulinzi na usalama August 20, mwaka huu, walikamata kete 560
zinazodhaniwa kuwa dawa za kulevya.
Wakati huo huo, Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe: Dkt Ali Mohamed Shein, mara baada ua kuweka jiwe la
msingi skuli Chimba wilaya ya Micheweni aliwapongea wananchi hao kwa
uamuzi huo wa kujenga skuli kwa nguvu zao.
Alisema uamuzi wa kujiletea maendeleo ndio unaofaa kuungwa mkono na
kuigwa na kila mmoja, kwani maendeleo hasa ya sekta ya elimu inategemea
pia nguvu za wananchi.
“Mimi niwapongeze wananchi wa Shehia ya Chimba kwa uamuzi sahihi na
adhimu wa kuwajengea watoto wenu skuli ya karibu na sasa masafa ya
kilomita sita yatawaondoka”,alieleza.
Hata hivyo Rais huyo wa Zanzibar amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa kaskazini
Pemba, kuzipitia skuli zote za mkoa huo, na iwapo atabaini kuna waalimu
watoro atoe taarifa kwa waziri wa elimu ili wafukuzwe kazi.
“Wapo waalimu kwanza ni watoro skuli na hujifanya wanaumwa, lakini
hawaendi hospitali na hujikalia nyumbani na wanakula mshahara, waripoti
na kisha wafukuzwe kazi”,alifafanua.
Akisoma risala ya ujenzi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya
Micheweni Hamad Mbwana Shehe alisema, ujenzi huo wa madarasa matano na
ofisi mbili za waalimu, umeshagharimu shilingi million 37.35.
Alisema kati ya fedha hizo shilingi 600,000 ni nguvu za wananchi,
shilingi 900,000 ni mchango wa Jumuia ya Maendeleo Tumbe, shilingi
3,500,000 kutoka Halmashauri, wakati mfuko wa jimbo wa mwakilishi na
mbunge jimbo la Tumbe umechangia zaidi ya shilingi 31.4.
Aidha amesema kwa sasa wanahitaji zaidi ya shilingi million 17,
534,000 kwa ajili ya milango, madirisha, rangi, dari na vyoo, ili
wanafunzi waanze kuitumia.
Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na
wajumbe wake, ataendelea na ziara yake ya siku tano asubuhi wilaya ya
Wete kwa kukagua shughuli mbali mbali za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na
uzinduzi wa kituo cha afya cha mama na mtoto cha Junguni.
chanzo: zanzibar24.
Comments