Alisema, vyama hivyo havikuanzishwa kwa ajili ya wachache kwenda
kwenye mikutano, makongamano na semina kujipatia fedha, bali ni kujenga
misingi imara na endelevu katika kuwatetea wanachama wao.
Katibu tawala huyo, alieleza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku
mbili ya haki za binadamu, kwa wanachama wa vyama vya wafanyakazi,
yalioandaliwa na kufanyika Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi
la Pemba.
Alieleza kuwa, wafanyakazi hasa kwenye sekta binafsi, wamekuwa
wakikoseshwa haki zao na wakati mwengine kufanya kazi zao bila ya
kuangalia usalama wao, hivyo ni nafasi kwa viongozi hao kuyafuatilia
hayo.
“Mimi naamini vyama vya wafanyakazi kama vikiwa makini kweli kweli na
kufanya kazi zao kwa kuangalia misingi ya haki na sheria zinavyotaka,
basi vitawasaidia sana wanachama wao”,alieleza.
Katika hatua nyengine, Katibu tawala huyo wa Wilaya ya Micheweni
amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo, kuifanyia kazi elimu
watakayopewa, ili wapunguze manung’uniko miongoni mwao.
Mapema Mratibu wa mafunzo hayo Siti Habib Mohamed, alisema ZLSC,
iliamua kuwapatia mafunzo hayo wanachama wa vyama vya wafanyakazi, ili
kuwajengea uwelewa zaidi.
“Kituo chetu kimekuwa kikitoa mafunzo kwa makundi mbali mbali, lakini
na wanachama wa vyama vya wafanyakazi nao tukaona umuhimu wa kukutanao
nao”,alifafanua.
Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba,
ZLSC Fatma Khamis Hemed, alisema kituo kimekuwa kikihakikisha kila kundi
ndani ya jamii, linapata uwelewa wa masuala ya kisheria, ili wafanye
kazi zao kwa ufanisi.
Wakichangia mada hizo, washiriki hao walisema bado vyama vya
wafanyakazi havijatekeleza wajibu wake ipasavyo kwa wananchama wake,
ikiwemo kuwaelimisha.
Makame Suleiman alisema bado vyama hivyo vinahitaji ushawishi wa hali
ya juu, ili kwa wale ambao hawajajiunga waone umuhimu wake na faida.
Nae Marzuku Khamis Sharif, alisema lazima hata kwa wananchama wenyewe
waone umuhimu wa kujisomea sheria mbali mbali kwa faida yao.
Katika mafunzo hayo mada sita zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na
ufafanuzi wa sheria ya mahusiano kazini no 1 ya mwaka 2005, sheria ya
mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF no 2 ya mwaka 2005, sheria ya fidia,
sheria ya afya na usalama kazini no 8 ya mwaka 2005 na sheria ya uajiri
no 11 ya mwaka 2005.
chanzo: zanzibar24.
Comments