Hakimu wa Mahakama acharazwa mapanga Mtwara.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Halfani Ulaya, amejeruhiwa vibaya sehemu za mwili wake na majambazi akiwa nyumbani kwake usiku wa kumkia jana.

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Neema Mwanga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea juzi saa 2:30 usiku wakati hakimu huyo akiwa amelala nyumbani kwake maeneo ya Mtandi Kata ya Mtandi.


Kamanda Mwanga alisema kundi la watu watatu wakiwa na mapanga walivamia nyumba ya hakimu huyo kisha kuanza kuwasumbua watoto wake ambao walikuwa nje ya nyumba hiyo, na baada ya Ulaya kusikia sauti za watoto wake alitoka nje na kukutana na majambazi hao.

Alieleza wakati Ulaya akiwa katika jitihada za kuwaokoa watoto wake wakiwa mikononi mwa majambazi hao, walianza kumpiga kwa kutumia mapanga hayo na kumjeruhi katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Alisema moja ya maeneo ambayo hakimu huyo amejeruhiwa vibaya ni mikono. na baadae alifanikiwa kukimbia na majambazi hao walifanikiwa kutoroka.

Kamanda Mwanga alisema watu hao haijajulikana walikuwa na dhamira gani dhidi ya hakimu huyo na kwamba hawakuchukua mali yoyote ya hakimu huyo.

Alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye anashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na atakayebainika kuhusika atafikishwa katika mkono wa sheria.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hispitali hiyo, Dk. George Kumwembe, alithibitisha kumpokea hakimu huyo akiwa na majeraha na kupatiwa matibabu ya awali.

Dk. Kumwembe alieleza kuwa hakimu huyo kutokana na hali yake kutokuwa nzuri, alipatiwa rufani na kupelekwa katika Hospitali ya Peramiho ya mjini Songea kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
chanzo: zanzibar24.

Comments