Dk. Shein aliyasema hayo leo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) pamoja na uongozi wa Bodi hiyo ya Mapato katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.
Katika vikao vya leo, Dk. Shein kwa nyakati tofauti alikutana na Uongozi wa Wizara Fedha na Mipango, Bodi ya Wakurugenzi ya ZRB na uongozi wake, Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi na uongozi wake pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na uongozi wake.
Akitoa maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa ZRB imepiga hatua kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza azma ya ukusanyaji wa mapato hatua ambayo imezipelekea Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa kuweza kufanya kazi zake vizuri.
Dk. Shein alieleza matarajio yake kuwa ZRB itaendelea kupata heshima kubwa sambamba na maendeleo endelevu lakini jambo la msingi ni kwa wafanyakazi wa ZRB kuwa wawazi na waadilifu ili mafanikio zaidi yapatikane katika ukusanyaji mapato.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi na Uongozi wa Mamlaka hiyo na kueleza haja ya kukuza mashirikiano kati ya Mamlaka hiyo na Wizara kwa lengo la kuimarisha sekta ya uwekezaji.
Akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) pamoja na uongozi wake, ambayo iko chini ya Wizara hiyo, Dk. Shein alieleza alivyoridhika na jinsi ZSSF ilivyobadilisha mtazamo katika mipango yake ikiwemo miradi iliyoekeza na kutoa pongezi zake kwa mafanikio hayo.
Aidha, alisisitiza haja ya kuzizingatia sheria nyengine mbali na ile sheria ya Mfuko huo ili uirahisishie katika utendaji wake wa kazi huku akieleza umuhimu wa Bodi hiyo kuendelea kutoa ushirikiano na uongozi wa Wizara.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd aliutaka uongozi wa ZIPA kufuatilia miradi inayoipitisha na kutambua inafanya kazi kiasi gani.
Akitoa mchango wake kwa Mfuko wa ZSSF Balozi Seif alitoa pongezi kwa Mfuko huo kwa kuendeleza vyema mipango yake na kusisitiza haja ya kuwepo umakini kwa wakandarasi wanaowapa kazi za kuwajengea miradi yao.
Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk. Khalid Mohamed alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa miongozo mizuri anayoitoa kwa Wizara hiyo na ndio maana imekuwa chachu ya mafanikio ya ukusanyaji wa kodi.
Aliongeza kuwa suala la uadilifu limepewa kipaumbele na Wizara yake kwa wafanyakazi wa ZRB ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu na maelekezo wafanyakazi hao pamoja na kuchukuliwa hatua kwa wale wanaokwenda kinyume na maadili.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee kwa upande wake alisisitiza haja ya kuainisha aina ya uwekezaji unaotakiwa kuekezwa katika maeneo yaliotengwa ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Mwanasheria wa Zanzibar Said Hassan alisisitiza umuhimu wa kuifanyia kazi Sheria namba 4 ya ZIPA ambapo mbali ya sheria hiyo ni vyema kwa Mamlaka hiyo ikazifahamu sheria nyengine muhimu kwa upande wake ikiwemo Sheria ya Kampuni, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Kazi na Sheria ya Uhamiaji.
Mwenyekiti wa ZRB Saleh Sadik Othman alieleza kuwa Bodi hiyo ya Mapato Zanzibar katika kutekeleza mipango yake ya muda mrefu inakusudia kabla ya kufikia mwaka 2020 inahakikisha inakusanya TZS 800 Bilioni kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Alieleza kuwa ZRB imekadiriwa kukusanya mapato yenye jumla ya TZS 396.24 Bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ikilinganishwa na makadirio ya TZS 272.64 Bilioni ya mwaka wa fedha 2016/2017 kutokana na vianzio mbali mbali inavyovisimamia ambako kumekuwa na ongezeko la asilimia 45.33.
Aliongeza kuwa ili kuweza kufikia lengo la makusanyo ZRB itatakiwa kukusanya wastani TZS 33.2 bilioni kwa kila mwezi huku akisisitiza kuwa Bodi hiyo ya Mapato itaendelea na hatua za kupambana na magendo ya biashara ya mafuta kwa kushirikiana na vyombo vya usalama hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Nassor alieleza mikakati ambayo imewekwa na Mamlaka hiyo katika kuimarisha sekta ya uwekezaji hapa Zanzibar.
Nae Mwenyekiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar Dk. Suleiman
Rashi Mohamed alieleza mafanikio na malengo yaliofikiwa na Mfuko huo.
Nao uongozi wa Mfuko huo ulieleza hatua zilizofikiwa katika muendelezo ya miradi iliyopo na kueleza kuwa kwa upande wa Mradi wa ujenzi wa eneo la Michenzani mjini Zanzibar ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni na tayari uzio umeanza kujengwa.
chanzo:Zbc.
Comments