
Dk. Shein alitoa ahadi hiyo katika ziara yake ya kutembelea miradi ya
maendeleo sambamba na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2015-2020 inavyotekelezwa katika Mikoa yote ya Unguja na
Pemba, ziara inayoendelea Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambapo
vijiji hivyo vimo ndani ya Wilaya hiyo.
Akiwa katika kijiji cha Ukongoroni mara baada ya kukagua shamba la
kilimo cha midimu alipata fursa ya kuwaeleza wananchi waliofika katika
banda wanalohifadhia ndimu zao kuwa kutiwa lami kwa barabara zao hizo za
Ukongoroni na Charawe ni utekelezaji wa ahadi ya chama chake ambayo
aliahidi yeye mwenyewe.
Dk. Shein alisema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa
vifaa kwa Idara husika ya ujenzi wa barabara (UUB), juhudi za makusudi
zitachukuliwa katika kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwani tayari
ndani ya uongozi wa Serikali anayoiongoza imeweza kuijenga kwa kiwango
cha kifusi.
Aliwaleleza wananchi hao kuwa Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar
imefanya mambo mengi na kuwahaidi kuwa atahakikisha vijiji hivyo
vinazidi kupata maendeleo endelevu na kamwe vijiji havitokuwa kama
vilivyokuwa hapo siku za nyuma huku akiponmgeza kilimo cha ndimu
kinavyoendeshwa hapo Ukongoroni.
Akiwa kijiji hapo, Dk. Shein aliwataka Mawaziri husika ambao wananchi
walizitaja changamoto walizonazo kupitia Wizara zao wawahakikishie ni
kwa namna gani Serikali kupitia Wizara zao itazitatua changamoto hizo
zikiwemo barabara, afya, elimu, kilimo na sekta nyenginezo.
Ambapo kwa upande wa kilimo Waziri husika wa Wizara hiyo Hamad Rashid
Mohammed alieleza hatua zinazochukuliwa kupitia mradi wa MIVARF
kuwapatia mashine wakulima wa ndimu kwa ajili ya kuzisarifu ili hatimae
wapate soko la uhakika.
Nao wananchi wa kijiji cha Ukongoroni kupitia Sheha wao Haji Vuaa
Khamis walieleza changamoto zinazowakabili ikiwemo barabara yao yenye
urefu wa kilomita 13.7 kutaka kuweka lami pamoja na ile ya Charawe yenye
urefu wa kilomita 12.8, pamoja na uhaba wa madaktari.
Nao Mawaziri wasio na Wizara Maalum kutoka vyama vya upinzani
walipongeza juhudi za Dk. Shein za kuwapelekea wananchi maendeleo na
kuahidi kuwa wataendelea kumuunga mkono kwani maendeleo hayana chama
huku wakiwataka vijana kuiheshimu Serikali na kuyathamini Mapinduzi
matukufu ya Januari 12, 1964.
Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya Mkoa huo huko katika Ofisi za
Mkoa wa Kusini Unguja zilizopo Tunguu, Wilaya ya Kati ambapo taarifa
hiyo ilieleza mafanikio, changamoto na utekelezaji wa miradi ya
maendeleo katika Mkoa huo.
Taarifa hiyo ilitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuongoza
kwa busara, hekima na uadili huku wakipongeza hatua zake kwa kufanya
ziara hizo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote wa Zanzibar.
Wakati huo huo, Dk. Shein aliweka jiwe la msingi katika jengo la CCM
Tawi la Kaebona na kueleza kufarajika na ujenzi huo ambapo wanaCCM hao
watapata fursa ya kujadili mambo ya chama chao na kuahidi kuliezeka,
kuliweka milango, madirisha pamoja na kutoa mtaji kwa mradi wa duka lao
wanalolijenga tawini hapo.
Aidha, Dk. Shein aliweka jiwe la Msingi ghala la kuhifadhia mazao ya
JKU huko Cheju na kupongeza juhudi zizochukuliwa na kikosi hicho chini
la kuahidi kuzitekeleza changamoto zilizoelezwa zikiwemo kuwapatia
matreka pamoja na mashine ya kupandia mbegu.
Dk. Shein pia, alikihakikishia kikosi hicho kuwa Serikali
anayoiongoza itaendelea kutekeleza azma ya vikosi vya Serikali
vilivyoasisi na Rais wa Awamu ya kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid
Amani Karume.
Katika taarifa iliyosoma na uongozi wa JKU katika kambi hiyo ya Cheju
iliyoanzishwa mwaka 1976, ilioanzishwa kwa lengo la kuendesha kilimo
cha Mpunga wa kutegemea mvua yenye ukubwa wa ekari 85 ambazo 70
zinalimwa mpunga na kunde, 10 kilimo mchanganyiko na 5 kwa ajili ya
majengo.
Uongozi huo ulieleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa ghala hilo
umetokana na vianzio vya mapato ya miradi ya Kambi na sio ruzuku kutoka
Serikalini.
Akiwa Mitakawani, Dk. Shein alipata maelezo juu ya mradi wa maji safi
na salama pamoja na kukagua mradi wa kisima cha maji na kuitaka Mamlaka
ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja kisima hicho
kiwe kimekamilika ili wananchi wa kijiji hicho wapate huduma hiyo ya
maji.
Dk. Shein pia, alizindua Mradi wa kisasa wa ufugaji wa nyuki huko
Dunga na kupata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kati Mashavu Sukwa
juu ya mradi huo ambao Wizara ya Kilimo ulipeleka wataalamu na kuanza
kwa mitego mipya 13.
Alioongeza kuwa kwa kila mtego hupelekea kupatikana kwa lita kumi za
asali ambapo kila lita moja huuzwa kwa TZS elfu 20 hivyo kwa mara moja
mfugaji anapata laki 2 shughuli ambayo anaweza kuifanya mara moja kila
baada ya miezi miwili.
Pia, Dk. Shein alipata fursa ya kukagua kazi za ujasiriamali za
Baraza la Vijana wa Wilaya ya Kati na kupongeza juhudi zao
wanazozichukua katika kuendeleza miradi yao na baadae aliweka jiwe la
msingi la jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja.
Akitoa salamu zake mara baada ya kuweka jiwe hilo la Msingi, Dk.
Shein alipongeza hatua za ujenzi huo zilizofikiwa na Wilaya hiyo na
kueleza kuwa jengo hilo la ghorofa moja litamalizwa ili liwe la mfano
wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo: zanzibar24.
Comments