
Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti mara baada ya
kuvitembelea vijiji hivyo vilivyopo Wilaya ya Kaskazini A, ambapo
aliwataka Mawaziri husika wa sekta hizo kuhakikisha huduma hizo muhimu
zinawafikia wananchi hao katika kipindi hicho.
Dk. Shein alieleza kuwa kilio cha wananchi wa vijiji hivyo amekisikia
na kuwaahidi juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha huduma
hizo muhimu zinapatikana.
Alieleza kuwa si jambo sahihi kuwepo kwa baadhi ya wananchi hapa
Zanzibar kuendelea kukosa huduma hizo muhimu hivyo, alisisitiza kuwa
juhudi zitachukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanikiwa.
Nao Mawaziri wa sekta hizo pamoja na Mawaziri wengine aliofuatana nao
Dk. Shein, waliahidi kutekeleza agizo hilo kwa wakati na kutumia fursa
hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake anazozichukua katika kuwaletea
maendeleo wananchi wote wa Zanzibar bila ya ubaguzi.
Walieleza kuwa maendeleo hayana chama kwani yanamgusa kila mtu na
kusisitiza kuwa wao wakiwa viongozi licha ya kuwa baadhi yao si viongozi
kutoka CCM lakini watahakikisha wanamuunga mkono Dk. Shein na Serikali
yake katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Wananchi wa maeneo hayo walielezea kufurahishwa kwao na ziara ya Rais
wa Zanzibar na kueleza matumaini yao makubwa kutokana na ziara hiyo ya
Dk. Shein katika vijiji vyao na kufarajika na ahadi zake anazozitoa kwa
lengo la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Mapema Dk. Shein alianza ziara yake katika Wilaya hiyo ya Kaskazini
A, kwa kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Soko la Kinyasini na
kuwaeleza wananchi kuwa Serikali inayoongozwa na CCM kwa mashirikiano ya
washirika wa maendeleo ndio wanaojenga soko hilo na sio mwengine.
Dk. Shein alieleza kuwa wananchi walio wengi watafaidika na ujenzi wa
soko hilo kwa kupata ajira sambamba na kuwa na sehemu nzuri ya kufanyia
biashara ambapo maisha yataimarika kwa familia nyingi zitakazotumia
soko hilo.
Aidha, Dk. Shein alieleza kutoridhika kwake na hali ya baadhi ya
wafanyabiashara hivi sasa kuuza mazao yao pembezoni mwa barabara katika
eneo hilo la soko na kueleza kuwa jambo hilo sio muwafaka.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwahakikishia wananchi wa kijiji hicho
cha Kinyasini kuwa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Bububu
Mkokotoni ambayo itaanzia Chuini na kuwa si muda mrefu ujenzi wake
utaanza na kuweza kuwasaidia sana wananchi wakiwemo wa kijiji hicho na
maeneo mengine ya Mkoa huo.
Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na kupitia
Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za
Kifedha Vijijini (MIVARP) inayogharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ulieleza
kuwa mradi wa ujenzi wa soko hilo utagharimu TZS Bilioni 2.5.
Uongozi huo ulieleza kuwa soko la Kinyasini ndio soko kubwa kati ya
masoko yote yanayojengwa kupitia mradi wa MIVARF na kueleza kuwa kazi
inayoendelea hivi sasa ni ujenzi wa masoko ya Kinyasini Unguja,
Tibirinzi Chake Chake Pemba na soko la Konde na ukarabati wa soko la
mbogamboga Mombasa na ujenzi wa kituo cha mafunzo ya uhifadhi na
kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno huko Pujini Pemba.
Mara baada ya kuweka jiwe la Msingi na kupata maelezo katika kituo
cha uokozi na uzamiaji kiliopo Nungwi Dk. Shein alitoa pongezi kwa
kuanza vyema mradi huu wa ujenzi wa vituo vya uokozi na uzamiaji.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa Mkuu wa Kikosi hicho cha
KMKM kwa kukiendeleza vyema kikosi hicho huku akisisitiza kuwa nia ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni ya kukifanya kikosi hicho kuwa cha
kisasa zaidi.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Radhia Rashid Haroub alieleza
kuwa Mradi huo umeanza rasmi mwaka 2014/2015 na unatarajiwa kukamilika
mwaka 2018/2019.
Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo utajumuisha ujenzi wa vituo
sita ambapo hadi sasa kituo kimoja cha KMKM Kibweni kimekamilika na KMKM
Nungwi kimo katika hatua za mwisho.
Pia, umo ununuzi wa vifaa vya mawasiliano kwa vituo vyote tayari
umekamilika, utoaji wa mafunzo kwa wazamiaji 48 kati ya 62 yamekamilika
na mafunzo kwa wadau watumiaji bahari.
Pamoja na hayo, Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa katika kutekeleza
ununuzi wa Boti katika mradi huo Serikali imetenga TZS 2.1 Bilioni kwa
ununuzi wa boti mbili mpya za kisasa zenye uwezo wa kuokoa na kutoa
visaidizi 600 kwa wakati mmoja kwa chombo kimoja.
Katika ziara yake hiyo pia, Dk. Shein aliweka jiwe la msingi katika
Maskani ya CCM Tushikamane na kusalimiana na wanachama na wananchi
katika eneo hilo na kuahidi kutoa mchango wake kwa kuliezeka pamoja na
kuliweka madirisha na milango.
Akiwa katika eneo la Mkokotoni ambapo Serikali ina ampango wa kujenga
bandari kwa ajili ya vyombo vya usafiri wa watu pamoja na bidhaa, Dk.
Shein alipongeza hatua nzuri za matayarisho, bandari ambayo itakuwa na
urefu wa mika 170 na urefu wa mita 6.
Kabla ya kuangalia eneo hilo la Bandari, Dk. Shein alikagua na kupata
maelezo juu ya jengo la Ofisi ya Bandari hapo hapo Mkokotoni ambalo
tayari ujenzi wake umekamilika.
Kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa Shirika la Bandari, ujenzi wa
Bandari hiyo ya Mkokotoni hadi kumalizika kwake utakharimu jumla ya TZS
Bilioni 1.8 ambapo ujenzi wa nyumba hiyo ya Shairika hilo umegharimu
jumla ya TZS milioni 378.7.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo: zanzibar24.
Comments