Abiria wa bodaboda wasiovaa kofia ngumu Jijini Tanga wameanza kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kutozingatia usalama barabarani wakati wakiwa wamepanda pikipiki.
Jumla ya abiria 20 wamekamatwa wakiwa wamepanda pikipiki bila kuvaa kofia ngumu na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani huku waendesha bodaboda 152 wakishikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na makosa mbalimbali ikiwamo kutokuwa na leseni na bima.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alisema leo Jumanne kuwa oparessheni hiyo ina lengo la kudhibiti makosa yanayofanywa na waendesha bodaboda ya usalama barabarani ili kuounguza ajali zinazotokea.
Alisema oparesheni hiyo ambayo ilianza jumatano wiki iliyopita hadi Jana tayari madereva na abiria 172 wa bodaboda walikuwa wamekamatwa kati yao 20 wakiwa abiria wasiovaa kofia ngumu.
“Niwaambie tu kuwa oparesheni hii haitwaacha salama wasiofuata sheria za usalama barabarani,abiria wasikimbilie kupanda bodaboda bila kuvaa kofia watambue kuwa watakapokamatwa watawekwa rumande na hatimaye kufikishwa mahakamani,” alisema Wakulyamba.
Alisema kati ya waliokamatwa kuhusiana na oparesheni hiyo 10 kati yao tayari wamefikishwa mahakamani na wengine mashtaka yao yanaendelea kuandaliwa.
Wakati huo huo, watu watatu wakiwamo wanafunzi wamejeruhiwa baada basi la abiria aina ya Nisan Cravan linaotoa huduma ya daladala kati ya TangaBeach na Rascazone kuacha njia na kisha kupindukisha.
Kamanda Wakulyamba aliwataja waliojeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, kuwa ni Fahm Abdallah (9) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mzingani, Diana Msagati (19) mwanachuo wa Chuo cha Ualimu Sahare na Fatma Zindu (44) mkazi wa barabara ya 19 Ngamiani
jijini Tanga.
Comments