ZANZIBAR NA POTSDAM( UJERUMANI) KUBUNI MIRADI YA PAMOJA INAYOFANANA KIUCHUMI.

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar balozi seif ali iddi amesema ipo haja kwa miji ya zanzibar na wa potsdam wa nchini ujerumani kubuni miradi ya pamoja inayofanana kiuchumi ili iwanufaishe wakaazi wa miji hiyo.

Amesema hatua hiyo itazidisha ushirikiano uliopo katika kusimamia maendeleo ya wananchi wake.


balozi seif ali iddi alitoa ushauri huo wakati akizungumza na ujumbe wa viongozi wa manispaa ya potsdam iliyopo mkoa wa brandenburg nchini shirikisho la ujerumani ukiongozwa na meya wa mji huo bwana jann jackobs aliokutana nao ofisini kwake vuga mjini zanzibar.

Alisema faida ya ushirikiano baina ya miji ya zanzibar na potsdam kwa kipindi kirefu imeanza kuleta matumaini hasa ikizingatiwa ile miradi iliyoanzishwa kwa pamoja baina ya pande hizo mbili ya nyumba za maendeleo za kikwajuni { majumba ya mjerumani } pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya ujenzi wa mitaro ya maji machafu katika manispaa ya zanzibar.

Balozi seif alisema serikali ya mapinduzi ya zanzibar kwa upande wake itazingatia na kuona namna gani inaweza kusaidia nguvu katika uratibu wa uendelezaji wa ushirikiano wa utendaji wa kila siku wa miradi ya pamoja itakayoanzishwa na miji hiyo miwili.

Makamu wa pili wa rais wa zanzibar aliuomba uongozi huo wa manispaa ya potsdam unaoongozwa na bwana jann jackobs kuwa mbaalozi wazuri wa kuitangaza zanzibar kiuwekezaji nchini shirikisho la ujerumani.

Mapema meya wa manispaa ya potsdam bwana jann jackobs alisema mambo ya msingi ya ushirikiano kati ya mji wa potsdam na ule wa zanzibar yameshakubalika na tayari yanawekwa saini kipindi hichi kwa ajili ya utekelezaji wa pamoja.

Bwana jackobs alielezea faraja yake kutokana na sekta ya utamaduni na utalii kuanza kuonyesha matumaini ya mafanikio hasa katika baadhi ya matamasha yanayofanyika moja kati ya pande hizo kushirikisha wadau wa sehemu zote mbili.

Hata hivyo meya wa manispaa hiyo ya potsdan alifafanua wazi kwamba masuala ya mazingira na fursa za ajira hasa kwa vijana yanakusudiwa kufanyiwa utaratibu wa utekelezaji wake katika kipindi kifupi kijacho ili kuja kusaidia kustawisha maisha ya vijana wengi.

Manispaa ya potsdam iliyomo ndani ya mkoa wa brandenburg kilomita 15 kusini magharibi mwa mji wa berlin nchini shirikisho la ujerumani ina wakaazi wapatao laki 167,745 kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2015 ikilinganishwa na manispaa ya mji wa zanzibar yenye wakaazi laki 223,000 kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012.
chanzo:Zbc.

Comments