ZAFELA yazindua mradi wasaidizi wa sheria juu ya vitendo vya udhalilishaji Zanzibar.

Image result for ZAFELA ZanzibarMkuu wa Wilaya ya Magharibi B  Silima Haji Haji alisema ipo haja ya jamii kushirikiana ipasavyo kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa kuwatumia Wasaidizi wa  kisheria pale vitendo hivyo vinapotokea.
 
Akizungumza katika Mkutano wa Uzinduzi wa Wasaidizi wa Kisheria katika Wilaya ya Magharibi B, Mkuu huyo alisema iwapo kutakuwa na mashirikiano ya pamoja kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji bila shaka vitendo hivyo vitakwisha.
 
Alisema ni vyema Shehia zinazopatikana katika Wilaya hiyo anayoiongoza kuyaripoti matukio ya udhalilishaji kwa Wasaidizi wa kisheria ili watekeleze majukumu yao ikiwa ni pamoja na kushirkiana na Wanasheria katika kuzipekeka kesi mahakamani na kupatiwa ufumbuzi.
 
Alisema tatizo lililozoeleka ni jamii kuoneana muhali na kushindwa kuzipeleka kesi hizo  katika vyombo vya sheria jambo ambalo linapunguza kasi ya mapambano ya udhalilishaji.
 
Mkuu huyo wa Wilaya alisema uzinduzi huo umefanyika wakati muafaka ikiwa jamii bado inakabiliwa na tatizo la udhalilishaji na kwamba Wasaidizi wa Kisheria wataweza kulipunguza tatizo pale watakapopewa mashirikiano ya kutosha.
 
“Tukitumia sheria iliyopo tutafanikiwa kwani sheria ndio msingi wa utatuzi wa suala hili tujitahidi kushirikiana katika kutoa ushahidi” alisema Silima.
 
Alisema tabia iliyozoeleka kwa Jamii kuyamaliza nyumbani matatizo ya udhalilishaji ni jambo linalochochea kwa kiasi kikubwa Wanafamilia kuendelea kujihusisha na matukio ya udhalilishaji kwa kuamini kuwa hawatachukuliwa hatua za kisheria.
 
Alifahamisha kuwa ili kushinda mapambano dhidi ya udhalilishaji ambayo yamekithiri ni vyema kuondoa huruma na muhali kwa watu ambao wanahatarisha maisha ya watoto kwa kuwafanyia matendo hayo.
 
“Ukweli ni kwamba udhalilishaji umekithiri  hasa kwa watoto wa jinsia zote  tuwe na huruma kwa watoto wetu kuwafanyia vitendo hivi kwani mtoto ukimfanyia kitendo hicho unamvunjia maisha yake kwa kumuathiri kimwili na kisaikoloji hivyo tushikamane ili kuwashinda wale wasiowatakia mema watoto wetu”Alisema Silima.
 
Nae Katibu wa Umoja wa wanasheria Wilaya ya Magharibi B Bimkubwa Haji Kheir alisema uzinduzi wa Wasaidizi wa Sheria juu ya vitendo vya udhalilishaji katika Wilaya hiyo utawajengea uwezo mkubwa Wanawake na watoto kujua haki zao.
 
Akizungumzia kuhusu malengo ya uzinduzi wa mradi huo alisema ni pamoja na kuwashajihisha wanajamii kuweza kufahamu uwepo  wasaidizi wa sheria katika wilaya na pindipo ikitokea kesi ya udhalilishaji  kukimbiliana kuwapatia msaada wa kisheria.
 
Hata hivyo ameyazungumzia malengo waliyojiwekea ni kuwawezesha wanajamii kuifahamu na kuitambua sheria ya mtoto no 6 ya mwaka 2011 ili kuweza kusimamia na kuitekeleza kwa maslahi ya mtoto.
 
Pia kuimarisha mawasiliano kati ya serikali za mitaa na mitandao ya kijamii katika kukuza uelewa kwa jamii juu ya masuala ya maendeleo, matunzo na afya bora kwa mtoto.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA Safia Hija Abras alisema,  wanasheria wa zafela wamefarijika sana kuwepo kwa wasaidizi wa kisheria ndani ya wilaya hiyo kwani kutapelekea kuwasaidia akinamama wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji kupata urahisi wa kupeleka kesi zao kwa wasaidizi hao na kushughulikiwa kiharaka.
 
Uzinduzi huo wa Wasaidizi wa Kisheria katika Wilaya ya Magharibi B umefadhiliwa na LSF Ligo Service facilities kutoka Tanzania kwa msaada wa Shirika la Danida, Ukaid  kwa lengo la kutatua matatizo yanayowakabili kinamama na watoto pamoja na walemavu.
chanzo: zanzibar24.

Comments