WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitahusika na ulipaji wa deni la
fedha za Ushirika na badala yake kila aliyekula fedha hizo atazilipa
mwenyewe.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo jana (Jumatatu, Julai 10, 2017), wakati akizungumza
na wananchi wa wilaya ya Liwale katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye uwanja wa michezo wa wilaya.
Waziri
Mkuu ambaye yuko katika na ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi,
alisema Serikali haiwezi kukubali Ushirika ukafa nchini kwa ajili ya
watu wachache wasiokuwa waaminifu.
Alisema watu wote waliopewa dhamana ya kuongoza Vyama vya Ushirika na kuamua kujinufaisha kwa kula fedha za vyama watazilipa.
Waziri
Mkuu aliwaagiza Viongozi wa Mkoa wa Lindi kufanya ukaguzi katika Vyama
vyote vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili kubaini ni wakulima wangapi
wanadai.
Alisema
baada ya kufanya uchunguzi na kubaini idadi ya wakulima wanaodai na
kiasi cha fedha wawachukulie hatua wahusika wote kwa mujibu wa sheria.
Awali,
Waziri Mkuu alizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale
katika Ukumbi wa Tengeneza, ambapo amewataka Watumishi wa Umma Nchini
kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika utoaji wa huduma kwa
Wananchi.
Alisema
Watumishi wanawajibu wa kuwahudumia Wananchi bila ya kutengeneza
mazingira ya kuomba rushwa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za
kisheria.
Alisema
Watumishi wa Umma wanatakiwa kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia
maadili ya kiutumishi jambo litakaloondoa malalamiko kutoka kwa
Wananchi.
“Lazima
Wananchi waone na wanufaike na kazi inayofanywa na Serikali yao, hivyo
ni wajibu wa Watumishi kuwatumikia Wananchi popote walipo na si kukaa
maofisini.”
Pia aliwataka Watumishi hao kupanga mipango itakayoleta tija kwa Wananchi na si vinginevyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 10, 2017
chanzo:mpekuziblog.
Comments