Wauza miili na watumiaji dawa za kulevya vinara wa Ukimwi Zanzibar.

Tume Ya Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) leo wamesaini makubaliano yenye lengo la kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi, ili kupunguza  kasi ya ugonjwa huo unaoendelea kuleta athari katika jamii ikiwemo kupotea kwa rasilimali watu nchini.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kilichowajumuisha watendaji  wa tume hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa  Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania Dk. Leonard Maboko amesema utafiti unaoendelea umeonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15-19 ndio wanaoathirika zaidi na maambukizi mapya, hususani wanawake .


Akizungumzia hali ya maambukizi hapa Zanzibar Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya ukimwi Zanzibar Ahmed Muhammed Khatib amesema maambukizi hayo kwa asilimia kubwa yanatoka katika makundi maalumu ikiwemo Wanawake wanaouza miili yao , wanaume wanaojamiana bila ya kutumia kinga na  vijana waaotumia madawa ya kulevya hali inayochangia kuenea kwa ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti  wa Tume hiyo Dk. Hedwiga Swai amesema kikao hicho kitakuwa chachu ya maendeleo juu ya kuhamasisha wananchi kuitumia elimu wanayopewa na kutumia kinga wakati wa tendo la ndoa hususani vijana ili kupunguza viashiria vya ugonjwa wa ukimwi katika jamii.

Hata hivyo amesema  utafiti unaoendelea inaonesha idadi ya maambukizi imepungua ambapo kwa mwaka 2013 maambukizi hayo yalikua 72,000 na mwaka 2014 69,603 ,Mwaka 2015 48,000 na wito kwa jamii kuendelea kufuata taratibu za kiafya zinazotowa na wataalamu wa afya ili kujikinga na ugonjwa huo.

Naye Mwenyekiti Kamati ya Ushauri ya masuala ya UKIMWI, Afya ya kina mama na Watoto ya Taasisi ya Mabunge Duniani (IPU) Dk. Faustine Ndugulile amesema watahakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa mahitaji yaliyokusudiwa pamoja na kuwa na mpango endelevu ya kuwa na rasilimali fedha utakaowezesha kuondoa unyanyapaa kwa wagonjwa pamoja na vifo vinavyosababishwa na Ugonjwa wa ukimwi.

Dk. Ndugulile amesema wataendelea kuishauri serikali kuelekeza nguvu katika kuzisaidia taasisi na jumuiya zinazosimamia masuala ya ugonjwa wa ukimwi ili jumuiya hizo ziweze kufikia malengo waliyoyakusudia na kuwaokoa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.

 Mkutano huo wa siku mbili uliofanyika Maisara mjini Zanzibar ulihudhuriwa na wajumbe wa kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, watendaji wa Tume za Ukimwi kutoka Tanzania Bara na Visiwani ukiwa na lengo la kutafuta njia bora ya kuweza kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
chanzo: zanzibar24.

Comments