Wataalamu wa maji wa nchi 25 za Afrika wakutana Dar.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson
Kamati ya wataalamu wa maji kutoka nchi 25 za Afrika wamekutana leo jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kutekeleza mpango wa kuwafikishia wananchi maji.
Azimio namba sita la Umoja wa Mataifa (UN) linayataka mataifa yote kuhakikisha kwamba wananchi wao wanapata maji kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kamati hiyo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, amesema nchi za Afrika zilianzisha Baraza la Mawaziri wa Maji Afrika (Amcow) ili kusimamia kwa karibu utekelezaji wa azimio la UN.

Lwenge amesema kikao hicho cha wataalamu kitajadili mambo mbalimbali jinsi ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji na Septemba mwaka huu kamati hiyo itawasilisha ripoti yake kwenye Baraza la Mawaziri wa Maji Afrika.
"Kila nchi imeleta wataalamu wake kuja kueleza namna wanavyotekeleza utoaji wa huduma ya maji kwenye nchi zao. Sisi Tanzania nia pia tuna malengo yetu ya kuhakikisha kwamba wananchi wa vijini na mijini wanapata huduma ya maji safi pamoja na maji taka," amesema waziri huyo.
Lwenge ambaye pia ni Rais wa Amcow, amesema changamoto kubwa wanazokabiliana nazo ni baadhi ya nchi kutochangia baraza hilo lakini sasa mwamko umeongezeka na wameanza kuchangia.
Amewataka wadau mbalimbali wa maji kushirikiana na Serikali za Afrika katika kusaidia upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
chanzo:Mwananchi.

Comments