Katika kutekeleza mpango wa kupunguza makazi holela nchini, wananchi wametakiwa kuelimishwa ili watambue umuhimu na fursa mbalimbali za kimaendeleo zilizopo kupitia mpango huo.
Akizungumza leo Ijumaa Julai 7, wakati wa uzinduzi wa mradi wa upangaji na upimaji ardhi katika Kata ya Msigani iliyopo Wilaya ya Ubungo, Mkurugenzi wa mipango miji na vijiji katika Wizara ya Ardhi, Profesa John Lupala alisema kuwa urasimishaji unatoa fursa nyingi ikiwamo kumilikishwa maeneo na kuwaondolea hofu ya kuvunjiwa nyumba zao.
Alisema kuwa kwa mwaka huu wa fedha Wizara imejipanga kurasimisha na kutoa hati takribani laki 4 ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili wajue umuhimu wa urasimishaji.
"Suala la urasimishaji si kwamba tunataka kupima na kumilikisha maeneo bali tunaamini lengo kubwa la kimaendeleo ni kuwafungulia wananchi fursa watumie ardhi kama mtaji,"amesema Profesa Lupala.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Upimaji na Upangaji wa Makazi (HUSEA), Renny Chiwa amesema kuwa zoezi hilo linafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ndege (drones) zitumikazo kupiga picha na kuainisha maeneo.
Pia mradi huo utasaidia ukusanyaji wa mapato kupitia TRA ambapo watapata takwimu sahihi za makazi ili kusaidia kupanga kiasi cha tozo kulingana na jengo.
"Uendelezaji wa miji yetu kwa mfumo tunaoenda nao ni makazi holela kwa zaidi ya asilimia 80 wakati watu wanaishi kwa hofu pale watakapoona miradi inaendelea katika maeneo yao ikiwamo kubomolewa nyumba zao, "amesema Chiwa.
chanzo:Mwananchi.
Comments