Wakulima wa Bonde Weni Wete Pemba waelezea mafanikio ya kilimo chao.



Image result for kilimo cha Shahidi


WAKULIMA wa kilimo cha Shadidi katika bonde la Weni, Wilaya ya Wete, wanaendelea kupata matumaini ya kujikimu kwa chakula baada ya kulima na kupata mavuno zaidi ya mpunga wa umwagiliji maji msimu huu.

Wakulima hao walitoa maelezo kwa nyakati tofauti, wakati walipokuwa katika ziara ya uvunaji wa pamoja katika bonde hilo, huko Weni,  Mkoa wa Kaskazini Pemba.


Waliendelea kueleza kuwa, kilimo cha shadidi kwa sasa ndio mkombozi mkubwa kwa wanajamii kujitosheleza kwa chakula na kuondokana na hali ngumu ya maisha, jambo ambalo linawekana kufuatia uwepo wa wataalamu.

Mmoja kati ya wakulima wa kilimo cha Shadidi, Bonde la Weni, Maryam Rashid Issa, alisema kuwa, jitihada inahitajika katika kuendeleza kilimo cha mpunga, ili kupata tija kubwa kupitia mbegu kidogo zenye kutoa mavuno mengi.

‘’Tujitahidini wakulima wenzangu tusivunjike moyo, mavuno ni mazuri, mbegu kidogo lakini ndo kama mnavyoona, tunawashukuru wataalamu wetu wakati wowote tunaowahitaji wanaitika’’, Mkulima huyo alieleza.

Hata hivyo, mkulima kutoka bonde la Dobi, Haji Mohammed Rubea ,alieleza kuwa uhalisia unaonesha wakati wa mavuno, hivyo aliwataka wakulima wenzake kufanya ushindani wa mafanikio kwa kupeana taaluma waliopatiwa kuendeleza mafanikio kwa faida yao na vizazi vijavyo.

‘’Mimi sijui siku niliokwenda dukani tokea kuanza kilimo cha shadidi, mavuno ni mazuri na mengi pembe nalisikia tu’’, alisema mkulima huyo.

Akisisitiza uendelezaji wa kilimo hicho Afisa kilimo, Wilaya ya Wete, Makame Hamad Said, alisema kuwa, tofauti kubwa ya mapato inaonekana wazi kwa wakulima kutokana na mavuno wanayoyapata kulinganisha na kilimo cha kutegemea mvua.

‘’Mvuno ni mazuri sana, ni hatua nzuri kufikia tani saba kwa hekta, ambapo kilimo cha kutegemea mvua huwezi kufika hata tani moja pamoja na mvua nyingi zilizonyesha kwa msimu huu’’, Makame alieleza.

Sambamba na hayo, Afisa huyo alisema kuwa, hatua ya wakulima wa umwagiliaji maji imefikia pazuri kiasi cha kupewa kipao mbele kwa kupatiwa pembejeo za kutosha, ili kutoa motisha kwa wakulima hao.

‘’Mpunga kama mpunga ndio chakula chetu, kiasi kwamba nyumbani kama hakuja pikwa wali huona hakuja pikwa, tuendelee kuhamasishana kuhakikisha kilimo hichi kinaendelea hata kama hakuna wahisani tuendeleleze taaluma tulionayo tuone vipi inazalisha kwa faida yetu’’, afisa huyo alieleza.

Kwa upande wake, Afisa utafiti wa Kilimo Pemba, Khatibu Bakar Haji, alisema kuwa, kupitia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti wa kina kupitia kilimo shadidi kuna uwezekano wa kujitosheleza kwa chakula.

Sambamba na hayo, Afisa Mkuu Idara ya umwagiliaji maji, Mbarouk Ali Mgau, alisema imani yake ni kuwa, wakulima wengi wamepata mabadiliko baada ya kufuata maelekezo ya wataalamu, pamoja na kuwataka waliopata hasara katika mavuno kuendeleza jitihada zao, ili waweze kufikia malengo katika msimu ujao.

Mradi wa kuongeza zao la Mpunga, kwa kutumia mbinu ya kilimo cha shadidi cha mpunga kwa kuwajengea uwezo wakulima, Mradi wa kilimo cha shadidi umeanza miaka miwili iliopita kwa kuwapatia wakulima mbegu sahihi zenye uzalishaji mkubwa.

Kati ya mbegu kumi zilizofanyiwa utafiti, mbegu tano ndizo zilizofanikiwa kuchaguliwa na wakulima kutokana na uzalishaji wake ambazo ni, Subang, Supa BC, TXD 88, TXD306, Supa India.

Comments