Wakazi Mpanda wapewa miezi sita kupisha ujenzi wa reli.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngoyani ametoa miezi sita kwa wakazi wa Mpanda Mkoani Katavi kuondoka katika maeneo ya hifadhi za Reli ili kupisha maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwenye miundombinu yake.
Ametoa agizo hilo jana (Julai 10) wakati akizungumza na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo Mkoani Mpanda na kusema ni wakati sasa kwa wananchi kufuata sheria kwa kutovamia miundombinu hiyo.

“Ninatoa miezi sita kuanzia sasa, itakapofika Januari mwakani wananchi wote watakaokuwa ndani ya hifadhi ya reli watabomolewa nyumba zao kwa kuzingatia sheria zinazolinda miundombinu,”  amesisitiza Ngonyani.
Ngonyani ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mpanda kusimamia zoezi la wananchi kuhama na kuhakikisha kila aliyevamia miundombinu hiyo anabomoa nyumba yake kabla ya sheria kufuata mkondo wake.
Pia amewatahadharisha wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuzingatia maslahi mapana ya Taifa wakati wa kutafuta zabuni kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuunga mkono Rais John Magufuli.
Katika hatua nyingine Mhandisi Ngonyani amekagua barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM), Sumbawanga-Kanazi (75KM) na ameiagiza TANROADS Mkoa wa Rukwa kuweka mizani katika barabara zinazojengwa ili kudhibiti magari makubwa yanayozidisha uzito na kusababisha uharibifu kwa barabara katika mkoa huo.
“Ni wakati sasa wanaotoa huduma za usafirishaji wa mizigo kufuata sheria kwa kubeba mzigo wa uzito unaostahili sababu madereva hao hao wakienda nchi za jirani wanafuata sheria kwa umakini, SUMATRA simamieni utoaji wa leseni kwa magari ya abiria na mizigo kwa kuzingatia uzito wa magari ili barabara zetu zidumu,”  amesisitiza.
Naye Meneja wa TANROADS Rukwa, Mhandisi  Msuka Mkina amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa wakala utahakikisha mizani inawekwa sehemu za barabara  ili kubaini magari yanayozidisha uzito na kuyachukulia hatua za kisheria.
Waziri Ngonyani yupo katika ziara ya kukagua barabara, viwanja vya Ndege, ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu na madaraja katika Mkoa wa Katavi na Rukwa.
 chanzo:Mwananchi.

Comments