Makada wa CCM wanaogombea nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa wameanza kulalamika kuhusu utaratibu wa chama hicho kuwakataza kujitangaza au kufanya kampeni zozote.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina wakihofia kuenguliwa kuwania nafasi zao, baadhi ya wagombea wamesema wamenyimwa haki yao ya msingi ya kujulikana kwa wapigakura.
“Sasa wapigakura watanijuaje? Kwa sababu siruhusiwi hata kuandika kwenye ukurasa wangu wa Facebook kwamba nagombea, binafsi sijafurahia,” amesema mmoja wa wagombea anayewania nafasi ya uenyekiti wa CCM, Wilaya ya Ilala.
Mgombea mwingine wa uenyekiti wa UVCCM Taifa, amesema bila kuruhusiwa kujitangaza, itakuwa vigumu kwa wapigakura nchi nzima kumfahamu kiongozi wanayetakiwa kumchagua.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema hakuna mgombea anayeruhusiwa kupiga kampeni kabla ya wakati, kusambaza picha au vitu vitakavyomfanya akiuke kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya chama hicho.
Hivi sasa, wanachama wa CCM wanaendelea kuchukua nafasi za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama na jumuiya zake, shughuli itakayokamilika Julai 10.
Hata hivyo, mwenyekiti wa zamani wa Shirikisho la Vyuo Vikuu (CCM) mkoani Iringa, Mariam Fundi amesema kanuni za uchaguzi ndani ya chama hicho zilikuwapo.
Amesema usimamizi mkali uliopo ndiyo unaowafanya baadhi ya waliokuwa wamezoea kutoa rushwa kuona kama wameonewa.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Jimson Mhagama amesema mgombea atakayethubutu kutangaza nia, kutoa rushwa au kuwashawishi wapigakura kwa namna yoyote ile hatabaki salama.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Raymond Mwangwala amesema uchaguzi huo umelenga kuwapata viongozi waadilifu watakaokivusha chama hicho kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020, hivyo ni lazima wagombea kufuata taratibu na sheria zilizowekwa ikiwamo kutofanya kampeni kabla ya wakati.
chanzo:Mwananchi.
Comments