Vyuo vikuu nchini vimetakiwa kutengeneza mfumo mzuri utakaowawezesha wanafunzi wanaohitimu kuwa na vigezo vya kuingia kwenye soko la ajira.
Ushauri huo umetolewa baada ya kuwepo kwa ongezeko la wahitimu wa vyuo vikuu ambao wanashindwa kupata ajira kutokana na kukosa stadi muhimu zinazomuwezesha mtu kuajiriwa.
Kukabiliana na changamoto hiyo Wakala wa huduma za ajira Tanzania (TaESA) imeanzisha program ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ili kuwapa ujuzi na stadi zitakazowawezesha kupambana na changamoto zilizopo katika soko la ajira.
Ofisa Habari wa (TaESA) , Jamila Mbarouk amesema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa wanafunzi wengi wa vyuo wanashindwa kupata ajira kutokana na muda mwingi wa masomo yao kupata mafunzo ya nazaria pekee.
Amesema programu hiyo inayoendeshwa na TaESA kwa kushirikiana na Shirika la Kazi duniani (ILO) limeanzia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwapa mafunzo wanafunzi 100 wa mwaka wa kwanza.
“Tulichokiona ni kwamba kuna changamoto kubwa ya wanafunzi wa Tanzania kuwa na umahiri mkubwa katika mafunzo wanayopata darasani na kukosa stadi za kupata ajira. Hilo ndilo linalosababisha wengi wanaomaliza vyuo kuishia mtaani,”amesema Jamila
Amesema ni muhimu kwa walimu wa vyuo vikuu kujenga mifumo itakayowawezesha wanafunzi kujiamini na kujieleza mbele za watu ili wawe na ujasiri wa kujibu kwa ufasaha maswali wakati wa usahili.
Mmoja wa wanafunzi walioshiriki katika mafunzo hayo Glory Mlugo amesema program hiyo itamuwezesha kumjengea kujiamini na kuingia kikamilifu kwenye ushindani wa soko la ajira.
“Najua kuna ushindani mkubwa kwenye soko la ajira na taswira ninayoipata ni kwamba mafunzo haya yanaenda kunipa mwanga. Nimejipanga kuyafuatilia kwa umakini mkubwa ili ninapoingia kwenye ushindani niwe nimekalimika,”.
Comments