Ndugu Waandishi wa Habari
Kwa
heshima kubwa tunawashukuru kwa dhati na kwa uungwana wenu wa kuitikia
wito wetu wa kuwaomba kuhudhuria mkutano wetu huu ili kuzumgumza nanyi
kama ilivyo ada na kawaida na hatimaye muweze kufikisha ujumbe wetu kwa
jamii na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Wandishi wa Habari
Itakumbukwa
kuwa hivi karibuni katika moja ya Baraza la Idd El Fitri lililofanyika
katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijijini Dar es Salam, Rais Mstaafu wa
Awamu ya Pili na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Ali Hassan Mwinyi,
alitoa maoni yake binafsi baada ya kuutazama, kuudurusu na kuridhika
na utendaji wa Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John
Pombe Joseph Magufuli.
Ni
ukweli usiofichika wala kupingika kuwa maoni ya Mzee Mwinyi bila
shaka yoyote yatakuwa yamepata mshawasha baada ya kuvutiwa mno na
uchapakazi wa Rais Magufuli, pia maoni hayo hayakuwa ni uamuzi wala
shuruti kama ambavyo baadhi ya watu walivyokishilia bango na
kulishupalia suala hilo kwa mtazamo hasi.
Maoni
ya Mzee Mwinyi yalikuwa bayana au kwa lugha nyingine ni maoni
mubashara yanayoweza kumlazimisha kila binadamu mwenye akili timamu
afahamu kwa yakini alichotamka katika matamshi yake. Alichosema au
kushauri ni jambo lenye mantiki kulingana na mtazamo wake ambao kwa
hakika ulijiegemeza chini ya uhalisia wa mazingira ya nyakati na
utendaji wa Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli kwa kadri
unavyoonekana.
Kwa
bahati mbaya sana, eti wanaojiita ni wazee wa CHADEMA bila kufanya
tafakuri, uchambuzi wa maana katika dhana kamili yenye uyakinifu wa
jambo hilo, jana wakajikuta wakikurupuka, na kumuandama Rais Mstaafu
Mzee Ali Hassan Mwinyi bila ya kuwa na sababu za msingi kwa kumtolea
maneno yasiyo na kichwa wala miguu.
Tokea
Rais Dk John Pombe Magufuli aingie madarakani baada kuchaguliwa
kidemokrasia na wananchi mwaka 2015, sasa yapata miaka miwili, utendaji
wa Serikali yake ya awamu ya tano licha ya kumvutia kila mtanzania,
umeitikisa na kuamsha mjadala nchini, Afrika Mashariki, Afrika na Dunia
nzima .
Mjadala
ni kuhusu kipimo cha utendaji wake unaochukua nafasi pana katika vichwa
vya Magazeti ya nje na ndani, kwenye vipindi vya runinga na mitandao
ya kijamii, Kitaifa na Kimataifa yote ikiwa ni katika kuutazama
uadilifu wake, uwazi na uwajibikaji wa Serikali yake chini ya misingi
ya uzalendo.
Watu
mbalimbali wamekuwa wakijadili kutokana na kushawishika kwao Rais
Magufuli kuhusu umakini alionao, uchungu kwa nchi yake na watu
anaowaongoza akiwa na azma ya kupigania na kutetea maslahi ya umma huku
akitaka rasilimali za nchi kuinufaisha nchi na watu.
Hakuna
mtu au kiongozi wa ndani au nje ya chama tawala na nje ya nchi
waliotumwa wajadili wanavyojadili iwe kwa kumpongeza na kumsifu
kunakofanywa na watu hao.
*Ndugu Waandishi wa Habari*
Waswahili
wa kale na wahenga wana semi mashuhuri isemayo“Kizuri hujiuuza na
kibaya Hujitembeza”. Yaonekana ndivyo inavyotokea kwa walimwengu
wanavyoutazama na kuufuatilia uongozi wa Awamu ya tano chini ya Rais Dk
John Magufuli na Serikali yake katika mtazamo chanya wenye mafanikio.
Alichokisema
Mzee Mwinyi si kuwataka au kuwashawishi wananchi kufanya mabadiliko ya
Katiba hatimaye kumpa nafasi ya vipindi vingine vya utawala Rais John
Magufuli abaki madarakani kinyume na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania .
Matamshi
ya Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi aliyaweka bayana akiyatanguliza
utangulizi wa maneno adhimu na dibaji yaliosema nanukuulaiti nchi yetu
isingelikuwa si yenye kufuata utawala wa kikatiba, Rais Dk John
Magufuli alitosha na kufaa kuongoza nchi yetu kwa siku na miaka
mingine.
Umoja
wa Vijana ya CCM (UVCCM) hatuoni kama hilo ni kosa au baa, ama iwe mwao
au uonekane uchuro kutokana na maneno hayo. Mzee Ali Hassan Mwinyi ni
mweledi, mlinzi mzuri wa Demokrasia na mtu anaheshimu Katiba, Katu
hakusema na kutaka Katiba ibadilishwe ili Rais abaki madarakani kama
inavyopotoshwa kauli yake.
Ndugu Waandishi wa Habari
Hata
hivyo inaonyesha wanaojiita Wazee wa CHADEMA hawana kumbukumbu ya
kutosha. Wamesahau Rais wa Awamu ya Kwanza Baba wa Taifa marehemu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitawala kwa kipindi cha miaka 23
tokea mwaka 1961 hadi mwaka 1985.
Mwalimu
Nyerere hakutawala miaka 23 kwa lazima yake, nguvu za udikteta au
kutumia misuli ya ubabe, alitawala kwa matakwa, ridhaa, utashi na
maamuzi ya wana nchi wenyewe ndiyo waliomshinikiza na kumuomba kila
wakati abaki madarakani kila alipopania kujiuzulu na kumpisha mtu
mwingine.
Ifahakime
kuwa Nchi yoyote na mahali popote, dunia inahitaji ipate mtawala na
utawala wenye tija, manufaa na maendeleo yanayoonekana, kuwaridhisha au
kuwapendezesha na kuwanufaisha wananchi.
Kushawishika
na kuhamasika kwa wananchi na watu mbali mbali juu ya kazi nzuri
inayofanywa na Dkt. Magufuli nadhani imewakumba mpaka Viongozi wenye
nyadhifa mbali mbali katika Vyama Vya Siasa na makundi mengine. Mfano
siku za karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi na wanachama wa
Chadema wakiwemo madiwani sita kwa hiari na ridhaa yao wameamua kuachia
ngazi na kukikimbia Chadema wakirejea CCM kwa kuridhika, kutosheka na
utendaji wa Serikali ya Rais Dk John Magufuli.
Wanaojiita
Wazee wa Chadema ingelipendeza sana kama wangekuwa na mapenzi na chama
hicho wangalikaa chini kutafakari na kutathmini sababu ipi inayowafanya
wanachama, viongozi waandamizi na madiwani hasa katika Mkoa wa Arusha
wakikimbie chama hicho na kurejea CCM badala ya wazee hao kucheza ngoma
isiowahusu.
Ndugu Waandishi wa habari
Wote
hapa tunaelewa Katiba ya nchi si Quran wala Bibilia. Katiba imetungwa
kutokana na maoni, weledi na utashi wa watu. Na watu hao hao kwa kujali
kwao mahitaji na matakwa yao, wanaweza kugeuza chochote ndani ya
katiba kwa kujali maslahi yao na wala isiwe baa au muujiza.
Umoja
wa Vijana wa CCM unaamini ukishafikia hatua ya uzee wakati mwingine
unapoteza kumbukumbu muhimu, tunawakumbusha wanaojiita wazee wa CHADEMA
hakuna ushahidi unaoonyesha Mzee Mwinyi aliwahi kuwa na mpango wa
kutaka kujiongezea muda ili abaki madarakani kama ilivyodaiwa na genge
la Wazee hao. Kama mjuavyo kule Chadema kuna maprofesa wa kuzua hili
nalo Mzee Mwinyi wamemzulia na kumpakazia.
Ingalikuwa
Mzee Mwinyi alitamani kujiongezea muda ili aendelee kubaki madarakani
kwa wakati ule, angeweza kwa sababu uongozi wake uliwakuna na
kuwapendezesha mno wananchi mijini na vijijini na wala isingelikuwa ni
kazi kubwa ya kukubalika na kuungwa mkono .
Zipo
semi na hadithi nyingi zinazodai Mwalimu Nyerere katika Kitabu chake
cha Tanzania na Hatma ya Uongozi alikiandika kwa lengo la kuwalenga
viongozi aliowakusudia kuwapasha na kutaka wajisahihishe, kujisuta,
kujiuzulu au kujirejebisha.
Ukweli
ulivyo si hivyo, Mwalimu kama Mwalimu kitaaluma aliandikia Kitabu
chake kwa msukumo wa maono yake ili kuiasa nchi yetu, viongozi wa sasa
na wajao pia kuitazama hatma ya nchi yetu kiutawala, kidemokrasia na
kiutendaji bila kumlenga au kumdhamiria yeyote kama inavyodaiwa na
makuhani wa kuzua.
Ndugu zangu Waandishi wa habari.
Mtu
mwerevu siku zote anapotaka kumuasa mwenzake atoe kibanzi katika jicho
lake, kwanza huanza kutoa yeye boriti katika jicho lake. Kama tujuavyo
Katiba za baadhi za vyama vya Siasa vikiwemo vile vya Ukawa. Katiba zao
zinalalamikiwa kwa madai ya kuwa na udikteta.
Tumeshuhudia
mivutano ikirindima ndani ya vyama hivyo huku viongozi wa Vyama hivyo
wakigombana kwa sababu ya kulinda matakwa ya Katiba zao na baadhi yao
wamekuwa ni zaidi ya wafalme na masultani waliojenga himaya ndani ya
Vyama vyao huku wakiwa hawana ndoto wala fikara ya kuachia madaraka.
Wapo
wanachama wengine wamefukuzwa na hata kuvuliwa uanachama ndani ya vyama
vya upinzani kwasababu ya kutaka kuwania nyadhifa za juu ambazo
wakubwa hawataki ziguswe kwakuwa kushika nafasi hizo ni kunagusa
maslahi yao.
Wengine
wanadaiwa kupoteza maisha katika mazingira ya kutatatanishi kwa
kujaribu kwao kuchukua fomu za kuwania nafasi za juu huku wagombea urais
wengine waliohama toka vyama vingine walipojiunga na vyama hivyo
nyakati za asubuhi, jioni yake wakapitishwa kwa mbwembwe kuwa wagombea
urais kinyume na matakwa ya Katiba zao .
Ndugu Waandishi wa Habari
Mwisho
Umoja wa Vijana wa CCM tunawataka wazee maslahi wa Chadema waache
kulishwa maneno na kuwa wazushi na waongo, waache papara ya kujibu kila
wanachokisikia kwa kuchochewa na ushabiki baada ya kuoayiwa milungula na
bahashish na kukimbilia kuwadhalilisha viongozi waliolitumikia Taifa
hili kwa uadilifu na bidii na juhudi huku wakiongoza nchi kwa hekima,
busara kubwa zilizosaidia kuleta mageuzi kadhaa ya kiuchumi, kijamii
na kisiasa yalioacha alama ya utumishi wao uliotukuka kwa watanzania.
Tunaendelea
kuwaaminisha watanzania Chama Cha Mpainduzi ni chama kikubwa ndani
Afrika na duniani kwa ujumla hivyo siku zote hakifanyi makosa katika
kuwaletea viongozi makini, wenye upeo na uweledi wa hali ya juu.
Ahsanteni
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
chanzo:mpekuziblog.
Comments