Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema hapendi kukamatwa na vyombo vya
dola kwa kuwa mahabusu si mahala pazuri pa kuishi watu hususan wasiokuwa
na hatia, hata hivyo amesema kitendo hicho hakitamuogofya na kuzuia
harakati zake za kupaza sauti.
Lissu
ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na
wanahabari kuhusu matukio ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chadema
kukamatwa na vyombo vya dola, na kuwekwa mahabusu.
“Sipendi
kukamatwa mahabusu si pazuri, lakini inafikia hatua inabidi uamue kama
kwenda machinjoni ukiwa umenyamaza kimya au kuingia huku unapiga kelele
mataifa yasikie,” amesema.
Lissu
ambaye mpaka sasa ana kesi za jinai takribani nne katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, ikiwemo ya uchochezi, amedai kuwa baadhi ya
viongozi na watumishi wa umma wako katika hali ya hofu katika utendaji
kazi wao, huku akiwataka wananchi kupaza sauti ili hali hiyo iondolewe.
“Hofu
kila mahali, mahakamani na hata kwenye utumishi wa umma hakuna aliyeko
salama. Viongozi wa dini wako kimya wanadhani wako salama. Tunahitaji
kupaza sauti kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments