Hawa, hawakuwa tofauti na wale waliotuambia kuwa, mtegemea cha ndugu
hufa masikini. Yote kwa yote, kumbe kumiliki chako ni jambo la faraja,
maana unaweza kukitumia, kukipumzisha wakati wowote uupendao.
Na ndio maana kauli hizo na nyengine, zimekuwa zikirejewa mara kwa
mara na wanaharakati wanaopambaana na magwiji wanaowapa watoto mimba za
umri mdogo hapa Zanzibar.
Wanaharakati hawa wamekuwa wakisaka mwarubaini na tatizo hilo kwa
mtoto wa kike, miaka nenda miaka rudi, ingawa kikwazo wanachokumbana
nacho ni ukosefu wa mashine ya vina saba ‘DNA’ Zazibar.
Changamoto ya mashine hiyo, imeshabisha hodi serikali kuu, baada ya
wanaharakati hao na waathirika wa mimba za mapema kuwa na sauti moja kwa
muda mrefu sasa.
Mdau mkuu wa kadhia hizi Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania ‘TAMWA’ kimekua kikihaha kila kona ya dunia, kuona kundi hili
la watoto wa kike linakuwa huru kama yalivyo makundi mengine.
Afisa Miradi wa TAMWA ofisi ya Zanzibar, Asha Abdi Makame, anaesema
wamekuwa wakisaka, kwanza uwezo wa kuwafikia walengwa, ili kuwapa
taaluma ya kujikinga na kadhia hiyo.
“Sisi kama TAMWA kwanza tunatoa elimu ya athari za ndoa za mapema na
mimba za umri mdogo, lakini hata waandishi wa habari huwa tunawapa elimu
ili kuvitumia vyombo vyao kuelimisha hili’’,alisema.
Yeye anasema, TAMWA pamoja na shughuli zake nyengine, lakini suala la
kupiga vita mimba na ndoa za mapema, wamelipa kipaumbele cha pekee,
maana hata hivi karibuni baada ya kuhangaika wamepata mradi.
“Mfano wenzetu wa EU, wametufadhili ingawa tumeshirikiana na Shiriaka
la Kimatafa la Idadi ya Watu ‘UNFPA’ kuwa mradi wa kupiga vita mimba na
ndoa za mapema kwa watoto wa wasichana, sasa tunatarajia
mafanikio’’,alifafanua.
TAMWA inakiri kuwa ukosefu wa mashine ya DNA, ni moja ya ukuta mkubwa
wa kumaliza kesi za mimba za umri mdogo wa watoto wa kike, kutokana na
Zanzibar kutokuwa na mashine yake yenyewe.
Analalamika kuwa kuwepo kwa mashine hiyo hospitali ya Muhimbili
pekee, ni udhaifu mkubwa, kwa wale watoto wa kike waliopewa ujauzito na
kisha kesi zao zikahitaji ‘DNA mahakamani.
‘’Unajua nguo ya kuazimwa haiendewi ngomani, inaweza kuwa mwarubaini
wa kuzipunguza ama kuzimaliza kesi za mimba za mapema kwa watoto
wetu’’,alisema.
Aliekuwa Mdhamini Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba wakati huo
Al-baghiri Yakout Juma, anasema wanazo kesi zaidi ya 12 ambazo
zinaendelea kusota kwenye mahakama za Mkoa, zikisubiri kipimo cha ‘DNA’
kilichopo hospitali ya Muhimbili.
“Unajua zinapopelekwa ‘sampuli’ kwa ajili ya kipimo cha ‘DNA’
Hospitali ya Muhimbili, ni sawa na kusema ndio mtoto wa kike
ameshakoseshwa haki yake, maana matokea hadi kurudi ni zaidi ya mwaka
mmoja’’,anasema.
Mtoto wa kike (19) ambae anakesi katika mahakama ya Mkoa Chake chake,
tokea mwaka 2013, kwa sasa ameshajifungua na mwanawe anasoma skuli ya
maandalizi, ambapo kesi yake inasubiri matokeo ya ‘DNA’.
“Sina hakika kwamba kesi itatolewa hukumu, maana hata alienipa ujauzito ameshamaliza kusoma chuo, na sasa yuko Unguja, anakuja kila baada ya miezi miwili kughairishiwa kesi yake’’,anasema.
Nae muathirika wa mimba ambae amejifungua mwaka 2014 na tayari
sampuli ya damu imeshachukuliwa na kupelekwa Muhimbili, anasema hana
hakika sana kwamba kesi yake itamalizwa.
“Nasikia wapo wenzangu wana miaka zaidi ya minne bila ya matokeo
kurudi, sasa lazima Zanzibar iwe na ya kwake ili kupunguza foleni
mahakamani, na sisi tupate haki zetu mapema’’,alifafanua.
Yeye anasema kama serikali ya Zanzibar haina uwezo wa kununua mashine
ya ‘DNA’ ni vyema iwaombe wafadhili kama EU, UNESCO, DANIDA, WHO ili
wanunue, maana vyenginevyo wengine watakosa haki.
Fatma Marouz Kombo ambae ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuia Kuelimisha
Athari za Madawa wa Kulevya, Ukimwi na Mimba za Utotoni ‘JUKAMKUM’
Pemba, anasema mwarubaini pekee wa kuzimaliza kesi za mimba ni kuwepo
kwa mashine ya ‘DNA’ Zanzibar, ambayo ndio chaka la vyombo vya sheria
kwa sasa.
“Wakati umefika kwa serikali kununua mashine ya ‘DNA’ ili hawa
wanaowapa mimba watoto wetu, wasiwe na pakukimbilia, maana sasa wamekuwa
wakidunda mitaani, kwa vile hichi kipimo hakipo kwetu’’,aliweka wazi.
“Inaweza kuwa juhudi zetu za kutokomeza hilo zikawa butu, iwapo
serikali yetu haitoharakisha kumiliki mashine yake ya ‘DNA’ badala ya
kutegemea ilioko Muhimbili’’,alifafanua.
Ali Mbarouk Omar ambae ni Afisa Mawasiliano wa Klabu ya watoto Pemba
‘PCC’ anasema uwepo wa mwashine ya ‘DNA’ wahalifu wa kuwapa mimba watoto
watafikia mwisho.
“Lakini hata ukienda Dawati la jinsia la wanawake na watoto na
mahakamani, kesi nyingi zimelala sababu ikiwa ni kukosekana kwa kipimo
cha DNA, sasa ni kazi kwa serikali, kuinunua na kuondoa adha
hiyo’’,alifafanua.
Katibu wa Jumuia ya Kupunguza Umaskini na Kuboresha Hali za Wananchi
Pemba (KUKHAWA) Hafidh Abdi Said, anasema pamoja na ushahidi kukamilika,
bado tatizo la kukosekana kwa mshine ‘DNA’ ni changamoto nyengine
katika vyombo vya kisheria.
Hivyo vyombo vya sheria nchini, wametakiwa kuacha kisingizio cha
ukosefu wa kipimo cha vina saba ‘DNA’ na kuwaachia huru
wanaowadhalilisha wanawake na watoto, ikiwa ni pamoja na wanaowapa
mimba.
Afisa Mipango wilaya ya Chakechake Pemba, Kassim Ali Omar nae
akifungua kongamano la siku moja, la kupinga ukatili wa kijinsia,
lililoandaliwa na jumuia ya kimataifa ya ‘YUNA’ alipigia chapuo kuweko
kwa mashine hiyo hapa Zanzibar.
“Sio busara kwa vyombo hivyo, kupata kichaka cha ukosefu wa kipimo
hicho, na hatimae kuwaacha watoto wa wanawake, wakiwa wamedhalilika na
wakosaji, kudunga mitaani’’,anafafanua.
Akizungumza kwenye mdahalo huo, Mkuu wa Idara ya wanawake na watoto
wa Wizara ya uwezeshaji, ustawi wa Jamii maendeleo ya wanawake na watoto
Pemba wakati huo, Sara Khamis Salim, anasema wazazi wamekuwa
wakijitahidi katika malezi, ingawa watoto hubuni njia ya kuwatoroka.
Afisa mkuu wa dawati la jinsia na watoto la Polisi mkoa wa kusini
Pemba, Asha Talib, anasema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa,
katika kutokomeza kesi za udhalilishaji wa kijinsia.
Polisi kwa makusudi limeanzisha madawati zaidi ya 417 Tanzania, ili
kuhakikisha wanawake na watoto wanaishi bila ya ukatili, ingawa jamii
imekuwa ikiviza nguvu hizo kwa kutokuwa tayari kutoa ushirikiano.
Hivi karibuni Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai Jeshi la Polisi
wilaya ya Micheweni Pemba, Suleiman Khamis Juma, wakati akitoa mada juu
ya majukumu ya jeshi la Polisi, ukumbi wa Benjamin Mkapa Pemba, anasema
kuwa kushughulikia makosa ya udhalilishaji na ulawiti ni moja ya jukumu
la jeshi la polisi.
Chakufurahisha afisa huyo anaeleza kwenye kongamano hilo kuwa, jeshi
la polisi kwa sasa linamchakato wa kujenga maabara kubwa na ya kisasa
katika maeneo ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, kwa lengo la kupunguza
usumbufu na msongamano wa vipimo vya vinasaba DNA.
Mwanasheria wa serikali kutoka ofisi ya DPP Zanzibar ofisi ya Pemba,
Ali Haidari Mohamed, yeye anasema vitendo vya ubakaji na udhalilishaji,
vimekuwa vikishika kasi kubwa na kuwaathiri watoto kisaikolojia.
Lakini Mratibu wa shirika Action Aid Pemba, Omar Ali Salum, aliitaka
jamii kuacha tabia ya kusuluhishana wenyewe kwa wenyewe, pale
zinapotokea kesi hizo na badala yake kuzifikisha kwenye vyombo vya
sheria.
Naibu Katibu Mkuu wizara inayoshughulikia wanawake na watoto Zanzibar
Mauwa Makame Rajab, anasema wazo la wanaharakati la kutaka serikali
inunue mashine hiyo ni jambo jema, na sasa hilo linatarajiwa kufanyika.
‘’Unajua kuwa zipo kesi nyingi mapaka waathirika wanakata tamaa na
watoto wetu kupewa ujauzito, sasa ni kweli Serikali ifanye hima kuwepo
kwa mashine hiyo’’,alifafanua.
Tokea mwaka 2011 hadi mwezi mwaka 2017 Dawati la Polisi mkoa wa
Kusini Pemba lilipokea kesi 10 za mimba, kwa ajili ya kupatiwa kipimo
vya ‘DNA’ na hadi mwaka 2014 ni mbili zilizorudi na nyengine zikiwa
foleni kusubiria kipimo hicho.
Mambo hayo ni tofauti kwa jamii ya leo, na ndio maana wapo watoto wa
kike 196, kati yao 122 wameripotiwa kupewa ujauzito na 74 kuolewa wakiwa
chini ya umri wa miaka 18.
Idadi hiyo ni ile kuanzia mwezi Januari mwaka 2012 hadi mwezi Disemba
mwaka 2016, tena hali hiyo ni kwa wilaya za Chakechake na Mkoni pekee.
Uchunguzi ukabaini kuwa, kwa mwaka 2012 pekee, kesi za mimba za
utotoni zilikuwa 73, wakati kipindi cha mwezi Januari hadi disemba 2014,
ziliripotiwa kesi 49 za mimba kwa wanafunzi.
Kesi za ndoa kwa wanafunzi, kulikuwa na idadi ya 54, kwa mwaka 2012
na mwaka 2016 kuliripotiwa kesi 20 katika taasisi mbali mbali.
Wizara ya elimu pekee ilikusanya jumla ya kesi 67 za mimba na ndoa,
ambapo kati ya hizo, mwaka 2012 kesi za ndoa zilikuwa 38, wakati kesi za
mimba kwa wanafunzi zilikuwa 14, wakati mwaka huu kumesharipotiwa kesi 9
za ndoa na 6 za mimba.
Vyanzo mbali mbali vya habari, vilisema chanzo cha kujitokeza kwa
matendo hayo husababishwa na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
mashine ya DNA Zanzibar.
Sheha wa shehia ya Madungu wilaya ya Chakechake, Mafunda Hamad Rubea,
aliweka wazi kuwa, KAIMU Naibu Mkurugenzi wa maendeleo ya ‘TEHAMA’
kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ‘TCRA’ Mhandishi Nehemia
Mwenisongole akielezea namna ambavyo, mteja wa kampuni moja ya simu
anavyoweza kuhama kutoka kampuni hiyo na kuhamia nyengine kwa namba yake
ile ile ya simu, wakati akizungumza na waandishi wa habari kisiwani
Pemba.kama Serikali ikinunua mashine yake, sasa watoto wa kike watapata
haki zao kwenye kesi za mimba na ubakaji.
Mrajisi wa Elimu Zanzibar Siajabu Suleiman Pandu, anasema ukosefu wa
mashine ya ‘DNA’ kwa Zanzibar ndio kikwazo pekee, maana mtoto wa kike
huathirika mara mbili na wa kiume mara moja.
“Mtoto wa kike kwanza kesi yake huchelewa maana hata samapuli ya vina
saba ikija, mwenzake ameshasahu machungu yeye bado, sasa lazima tuwe na
yetu Zanzibar’’,alisema.
Shirika la Kimataifala Kuchangia Maendeleo ya Mtoto, limeeleza kuwa,
wasichana zaidi ya milioni 14 huolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18,
katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara, nchi za Chad, Niger na Mali
zinaongoza.
Azimio la Umoja wa Mataifa la kupunguza aina zote za udhalilishaji
kwa wanawake (CEDAW) haliruhusu watoto wenye umri wa chini ya miaka 18
kuolewa.
Azimio la Haki za Binaadamu (the 1948 UDHR) linasema kwamba ndoa
yoyote nilazima iwe ni ya maridhiano na kwamba mtoto mwenye umri chini
ya miaka 18 huwa hana maamuzi huru.
Kila mwaka, watoto milioni 7.3 wa kike chini ya umri wa miaka 18
hushika na kujifungua mimba, imesema ripoti mpya kuhusu hali ya idadi ya
watu mwaka 2013, ambayo imetolewa na Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu
katika Umoja wa Mataifa, UNFPA.
Ripoti hiyo imesema, milioni 2 kati ya watoto hao wana umri usozidi
miaka 14, na kwamba watoto hao hukumbana na matatizo ya muda mrefu ya
kiafya na kijamii kutokana na mimba hizo, yakiwemo vifo vinavyohusiana
na uzazi.
Katika kukuza kampeni dhidi ya mimba za utotoni, na unyanyasaji kwa
watoto, UNFPA nchini Tanzania, limeshiriki katika mashindano ya riadha
ya Kilimanjaro Marathon nchini humo.
Hata hivyo aliekuwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa
Mamboya mwezi Julai mwaka 2011, alisema Serikali ina mpango wa kununua
mashine ya ‘DNA’ kutokana na umuhimu wake.
Alibainisha kuwa Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu kwa
kushirikiana na ofisi ya maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano Tanzania, pamoja na kutayarisha jengo la Mkemia Mkuu kwa
ajili ya kuweka mashine hiyo.
Aidha alisema DNA ni mashine ya kupima uasilia pale panapotokezea
utata wa mtoto, kipimo hicho hufanyika baada ya kuzaliwa mtoto na
kuthibitisha nani baba halisi.
Sasa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni kupitia waziri
wake katika afisi ya Makamu wa pili wa rais Zanzibar Mohamed Aboud
Mohamed, amesema tayari serikali imeshatenga shilingi bilioni 1 kwa
ajili ya ununuzi wa mashine hiyo.
“Sasa serikali imeshatenga bilioni 1 kutoka kwenye fungu la Mkemia
mkuu wa serikali kwenye mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 kwa ajili ua
kununua mashine ya DNA”,anabainisha.
Jengine linalotarajiwa kufanywa sambamba ni serikali imeshatenga
shilingi milioni 175 kwa ajili ya matumizi ya shughuli mbali mbali za
mapambano ikiwemo kuwaelimisha wananchi.
chanzo: zanzibar24.
Comments