Licha ya Serikali kuendeleza jitihada kadhaa kukabiliana na malaria, ugonjwa huo unaendelea kuwa changamoto nchini.
Hayo yamebainishwa leo (Julai 5) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya wakati wa kuadhimisha miaka 60 ya utendaji kazi wa Shirika la Afya la Amref Afrika.
Dk Mpoki amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau kutoka taasisi na mashirika mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo unaogharimu maisha ya watu wengi.
Amesema katika miaka 60 ya utendaji kazi wa Amref, imeweza kuwafikia wananchi wengi hivyo inaweza kutumia njia hiyo kushiriki katika vita ya kutokomeza malaria.
"Tunajitahidi kukabiliana na malaria lakini takwimu bado haziko vizuri, tunaomba wadau mshiriki katika vita hii, wenzetu Zanzibar wamefanikiwa," amesema.
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mahmoud Kombo amesema licha ya kufanikiwa kuyakabili maradhi kadhaa yakiwemo malaria na kipindupindu, changamoto imebaki kwenye kukabiliana na vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.
"Naumia sana kama waziri kuhusu jambo hili, vifo hivi vimekuwa vingi na bado watu wanaonekana hawana elimu ya kutosha. Nitumie fursa hii kuiomba Amref nayo ije kule itusaidie kuwafikia watu wa chini kabisa ambao kuna wakati wanaingia kwenye matatizo kwa sababu hawana elimu ya kuhusu jambo fulani," amesema Kombo.
chanzo:Mwananchi.
Comments