Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa imetoa wito kwa vijana wenye uwezo wa kubuni na kuchora kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye shindano ya kubuni nembo mpya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 5, msemaji wa wizara hiyo, Mindi Kasiga, amesema shindano hilo ni fursa nzuri kwa vijana kuonyesha uwezo wao, pia kujipatia kipato iwapo watashinda.
Mshindi wa kwanza atazawadiwa dola za Marekani 25,000 wakati atakayeshika nafasi ya pili atapewa dola 5,000 na watatu atapewa dola 2,500.
Shindano hilo limeanza Juni Mosi na litarajiwa kuhitimishwa Agosti 31, mwaka huu.
“Shindano hili limezinduliwa mwezi uliopita pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kigezo kikubwa kuwa kijana mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 ambaye anatoka katika moja ya nchi mwanachama wa Jumuiya,”amesema.
Alisema kuzinduliwa kwa shindano hilo UDSM haimaanishi kuwa shindano hilo linalenga wanafunzi pekee bali vijana wote wenye uwezo wa kubuni kwa njia yoyote na si lazima iwe ya kutumia kompyuta.
“Tunaomba vijana wengi wajitokeze kwa sababu sisi katika jumuiya hii tunafanya mambo mengi na tuna umuhimu, sisi tuna eneo kubwa kuliko nchi nyingine wanachama, makao makuu ya Jumuiya yapo kwetu,” amesema Kasiga.
chanzo:Mwananchi.
Comments