Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi awataka wasimamizi wa kodi kuwa waadilifu.

Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud  amewataka a wasimamizi wa kodi wakiwemo ZRB kufanya kazi kwa uadilifu ili kuzuia uvujaji wa Mapato kwa wafanya biashara.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya siku moja ya ukusanyaji mapato kwa kutumia Mashine za kielekroniki (EFDs) kwa Wakuu wa Mikoa,Wilaya na Makatibu tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Manispaa amesema nchi nyingi zinakuwa kimaendeleo kutokana na kufanikiwa kuhifadhi mapato ya kodi.


Hata hivyo amesema wakusanyaji kodi watakapo fanya kazi kwa uadilifu na  kufuata sheria wataisaidia serikali kutekeleza azma yake ya kufikia malengo waliyoyakusudia katika mwaka wa Fedha 2017/18 pamoja na kuwakamata wafanya biashara wote wanaokwepa kulipa kodi.

Akizungumzia matumizi ya Mashine hizo za EFD hapa Zanzibar, amesema mashine hizo zitasaidia kuondoa udanganyifu katika kulipa kodi kwa wafanyabiashara na kukusanya Fedha zilizokusudiwa kwa wakati na kutoa wito kwa wafanyabiashara kuendeleza utamaduni wa kulipa kodi ili nchi iweze kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Sera, Utafiti na Mipango wa ZRB Ahmed Haji Saadati amesema mbali na Mashine hizo kuhifadhi mapato yasipotee lakini pia zitasaidia kutunza kumbukumbu za mauzo na manunuzi kwa wafanya bishara ili kuondoa matatizo yanayoweza kujitokeza ikiwemo ukwepaji wa kodi kisheria.

Nao washiriki wa mkutano huo wameahidi kufikisha elimu hiyo kwa wananchi walio katika  shehia zao ili wananchi waweze kunufaika na kodi wanazotoa kwa kutekelezewa mahitaji muhimu ikiwemo Elimu, Afya na Miundombinu bora ya barabara.

Mashine hizo za EFD zinataraiwa kutumika hapa Zanzibar ifikapo mwezi November ili kuimarisha mapato yatokanayo na wananchi ikiwemo wafanya biashara kwa lengo la kuimarisha  maendeleo ya nchi.
chanzo:zanzibar24.

Comments