Miswada Mipya: Ni Marufuku kwa kampuni za madini kuweka fedha nje......Kesi Zote za Mikataba Zitaamuliwa Nchini.
Sasa
kampuni za madini zinazofanya kazi zake nchini hazitaruhusiwa kuhifadhi
fedha nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia mashauri ya
mikataba hiyo yatafanyika ndani ya nchi na siyo katika mahakama na
mabaraza ya nje, Bunge limepitisha katika kulinda rasilimali za nchi.
Akiwasilisha
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili
wa Mwaka 2017, Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi
alisema sheria inaeleza kuwa mapato yote yanayotokana na rasilimali na
maliasili na utafutaji, uchimbaji au umiliki na utumiaji wa rasilimali
za Taifa, yanahifadhiwa katika taasisi za kifedha za ndani ya Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania.
“Itakuwa
ni kosa kuweka fedha hizo nje ya nchi isipokuwa gawiwo ambalo mwekezaji
ataruhusiwa kutoa nje ya nchi kwa mujibu wa sheria za nchi za
Tanzania,” alieleza Profesa Kabudi na kuongeza kuwa pia sheria
inatamka kuwa mashauri kuhusu maliasili na rasilimali za nchi chini ya
mamlaka ya nchi hayatafanyika chini ya mahakama na mabaraza ya nje.
Aidha,
alibainisha kuwa sheria itatumika pande zote mbili za Muungano, bila
kuathiri mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya usimamizi
wa rasilimali za nchi.
Alisema
muswada huo pia unazuia usafirishaji wa maliasili bila kuongeza
thamani, lengo ni kuleta maendeleo na kutekeleza azma ya serikali ya
kuwa na Tanzania ya viwanda.
Akiwasilisha
Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika
Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017, Profesa Kabudi alisema
unawezesha wananchi kupitia Bunge, kupitia mikataba inayohusu rasilimali
na malisiali ya nchi ambayo imefungana na Jamhuri ya Muungano kwa lengo
la kujiridhisha kama masharti, makubaliano na mikataba haina masharti
hasi na yanakinzana na maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla na
kuishauri serikali.
“Sheria
imeipa nguvu bunge kupitia mikataba yote inayohusiana na malisili za
nchi na rasilimali zake iliyoingiwa na Jamhuri ya Muungano ili
kujiridhisha masharti yaliyomo kwenye mikataba hiyo yamezingatia maslahi
ya Watanzania.
"Na
endapo mikataba haitii maslahi ya Watanzania, basi Bunge liweze
kuishauri serikali kufanya majadiliano na wahusika wengine katika
mikataba kwa lengo la kuondoa masharti hasi yasiyokuwa na manufaa kwa
Taifa,” alifafanua.
Aliongeza
“Endapo itapita kuwa sheria, serikali haitafikia makubaliano yenye tija
kwa wananchi na taifa ndani ya muda utakaokubaliwa na pande zote basi
masharti yote hasi yatachukuliwa kwamba yamefutwa, na si sehemu ya
mikataba, na serikali haitakuwa na wajibu wowote wa kutekeleza masharti
ambayo yamebainika kuwa hasi.”
Profesa
Kabudi alisema serikali itapitia mikataba yote ya madini ya sasa kwa
kuzingatia sheria mpya zitakazopitishwa na Bunge katika Mkutano wa
Bajeti unaoendelea.
Alisema mikataba yote ya madini iliyopo sasa itapitiwa upya kwa kuzingatia sheria mpya zitakazopitishwa na Bunge.
“Miswada
hii inalenga kuleta mapinduzi makubwa katika kulinda rasilimali na
maliasili ya nchi, dhana ya miswada hii ni ukombozi wetu na mapinduzi ya
Watanzania wote,” alieleza Profesa Kabudi na kusisitiza umuhimu wa wabunge kupitisha miswada hiyo.
Alinukuu insha ya falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema, “Mapinduzi
haya yanayotakiwa ni kwa wote na si kwa wachache, tulipoonewa tulionewa
wote, tuliponyonywa tulinyonywa wote, tulipopuuzwa tulipuuzwa wote, ni
unyonge wetu sote kwa pamoja ndio uliotufanya tukaonewa, tukanyonywa na
kupuuzwa, mapinduzi tunayoyafanya sasa, ni lazima yawe yetu kwa pamoja
ili Mtanzania asiwe mnyonge, na unyonge wake ukatumiwa kumnyonya, na
kupuuza.”
Kambi ya Upinzani
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imepinga kitendo cha Serikali au Bunge
kutumia kifungu cha 5 (2) cha muswada muswada wa sheria ya mamlaka ya
nchi kuhusiana na umiliki wa maliasili wa mwaka 2017 ambacho kimeweka
umiliki wa rasilimali na maliasili za nchi mikononi mwa Rais kwa niaba
ya wananchi wa Tanzania.
Kambi
rasmi bungeni imesema kuwa kifungu hicho ni hatari ambacho kinaweza
kuleta madhara makubwa kwa taifa kisipoangaliwa kwa nidhamu ya hali ya
juu na kwa uzalendo uliotukuka kwani endapo anaweza kupatikana rais
ambaye si mzalendo nchi inaweza kutumbukia pabaya.
“Mikataba
hii imezipa kinga kubwa sana kampuni za madini ambazo zimesaini
mikataba na serikali na ikiwa ni pamoja na kuzuia kutumika kwa sheria
mpya ambazo zinapitishwa na Bunge kwa kampuni hizo kuanzia mikataba hiyo
inaposainiwa,” yalikuwa maoni ya Upinzani yaliyosomwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso.
Akichangia,
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) alisema Bunge
linapotunga sheria ni wakati muhimu wa kuwa makini na kwamba miswada
hiyo ilihitaji muda wa kutosha.
Alisema anataka kuamini kuwa Rais aliyepo ni mzalendo na anapenda watu. “Najiuliza
kwa mamlaka aliyopewa Rais siku akija mtu si mzalendo kama Magufuli
nataka kuamini hivyo akatokea hata upande huu hata Chadema kwa sababu
huku hakuna malaika au akitokea CUF nako hakuna malaika, akatokea rais
sio mwaminifu na amepewa mamlaka kubwa ya kusimamia rasilimali basi
atauza taifa hili,” alieleza Lema.
Mbunge
wa Geita Vijiji, Joseph Msukuma (CCM) aliwashangaa wabunge wanaopinga
miswada hiyo kuletwa kwa hati ya dharura na kuhoji kuwa mbona mgombea wa
urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa alipatikana kwa hati ya dharura.
“Hata
mgombea urais wa upande mwingine (Chadema) walipata mgombea kwa hati ya
dharura, walimuona anafaa kwa dharura waliyokuwa nayo, walimpata bila
kumchunguza huku wakijua kuwa walileta mtu ambaye wanataka akabidhiwe
nchi, na hajui chochote kuhusu Chadema na wananchi hawakuwahoji,” alisema.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments