Wizara ya Nishati na Madini, imepiga marufuku wachimbaji wa madini ya Tanzanite, Mererani wilaya ya Simanjiro, kusafirisha madini kutoka migodini bila kupewa vibali na maafisa wa wizara hiyo.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma amesema leo kuwa, wizara hiyo imechukuwa hatua hiyo ili kudhibiti matukio ya utoroshwaji wa madini hayo.
"Kuanzia sasa tumepiga marufuku kusafirisha madini bila kutoa taarifa kwa maafisa wetu waliopo Mererani na kupata vibali na ambao watakamatwa wakitoa madini kinyemela tutawachukulia hatua," amesema.
Akizungumzia taarifa ya kuibwa ndoo ya madini katika Mgodi wa Tanzanite One, Juni, 21 mwaka huu, Juma alisema kamati ya wajumbe sita aliyoiunda imebaini kuwa hakuna madini yaliyoibiwa.
Amesema kamati hiyo ya wataalam, iliongozwa na Ofisa Madini Mkazi wa Mererani, Elias Muterani.
Amesema kamati hiyo imefanya uchunguzi kama kuna upotevu ama kupungua kwa madini yaliyohifadhiwa katika mgodi huo, ambao unamilikiwa kwa ubia na Serikali kupitia Kampuni ya Taifa ya Madini (STAMICO) na Kampuni ya Sky Associate na kubaini hakuna upotevu wala kupungua.
"Lengo letu ni Serikali kujiridhisha na madini yote yanayotoka Mererani na tumeimarisha ulinzi katika eneo lote la Mererani," amesema.
Akizungumzia uvumi wa kuibiwa madini katika mgodi huo, mtaalam wa miaka kutoka Stamico, katika mgodi huo, Agrey Gonde amesema, baada ya kupata taarifa ya wizi walifanya ukaguzi katika eneo la hifadhi ya madini na kubaini hakuna wizi.
"Tumepima na kuhakiki ndoo zote zenye madini na hakuna wizi ambao tumebaini kwani Serikali pia imeimarisha ulinzi katika mgodi huo," amesema.
Naye Mkuu wa Ulinzi wa Tanzanite One, Abubakar Lombe alisema si jambo rahisi kuibwa madini katika mgodi huo kama ambavyo taarifa zinasambazwa.
Tukio hili limekuja wakati tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano likiwa limeshaunda kamati ya wabunge tisa kuchunguza sekta ya madini ya Tanzanite, kamati ambayo itafanya kazi kwa mwezi mmoja.
chanzo:Mwananchi.
Comments