Mahakama ya Dodoma imewahukumu kwenda jela miaka 32 kila mmoja washtakiwa saba baada ya kuwakutwa na hatia katika makosa matatu ya ujangili ikiwemo kuunda genge la uhalifu.
Hata hivyo, katika hukumu hiyo ambayo imesomwa na Hakimu Mwajuma Lukindo,haikumtia hatiani Boniface Malyengo (maarufu kama shetani hana huruma)baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha pasipo shaka mashtaka dhidi yake.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Malyango, Juma Malyango, Lucas Hosea, Mwinyijamal Igonza, Lucas Mayai, Emmanuel Sindano, Daud Mwaja na Yohana Chamaulaya.
Akisoma hukumu hiyo, Mwajuma amesema kuwa katika shtaka la kwanza lililokuwa ni kuunda genge la wahalifu, watuhumiwa saba walikutwa na hatia na kuhukumiwa miaka 10 jela huku Malyengo akiachiwa huru baada
ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha shtaka hilo.
Katika shtaka la pili washtakiwa sita wamekutwa na hatia ya kupatikana na nyara za Serikali na kuhukumiwa kwenda jela miaka miwili jela isipokuwa Malyango na Daudi Mwaja ambao upande wa mashtaka umeshindwa kudhibitisha.
Hakimu Mwajuma amesema katika shtaka la tatu watuhumiwa sita walihukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja isipokuwa Malyango baada ya kukutwa na shtaka la kukutwa na meno tembo 18.
Mwajuma ameamuru bunduki tatu zilizokamatwa katika matukio hayo na meno 18 zirejeshwe serikalini.
Hata hivyo, amesema hukumu hiyo itatakiwa kuthibitishwa na jaji wa mahakama kuu.
Awali Wakili wa upande wa Serikali, Salim Msemo aliiomba mahakama kutoa adhabu kubwa kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa jamii.
Hata hivyo, Wakili wa upande wa utetezi Paul Kusekwa ameomba mahakama
kuwapunguzia adhabu kwasababu washtakiwa hao wamekaa kwa muda wa miaka mitatu rumande.
“Kuwapa adhabu kali si lengo la kuwabadilisha ili wawe watu wema bali ni kukomolewa,”amesema Kusekwa.
Amezungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali Msemo alisema kuwa wataipitia hukumu hiyo ili kubainisha maeneo ambayo wameridhika nayo ama kutoridhika nayo na kisha kufuata taratibu za kisheria.
chanzo:Mwananchi.
Comments