Watoto mapacha walioungana wameanza rasmi kufanyiwa vipimo mbalimbali leo na jopo la madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kuangalia hali zao kiafya na iwapo kuna uwezekano wa kutenganishwa.
Akizungumza na Mwananchi leo, muuguzi kiongozi wa jengo la wazazi, Susana Ndamala amesema watoto hao walipokelewa Julai 24 mwaka huu na kuanza kupatiwa matibabu.
"Walipofikishwa hospitalini hapa waliwekwa katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU) na mama amelazwa katika wodi namba 36 ili kuwahudumia watoto wake," amesema Ndamala.
Amesema tangu wamempokea ameendelea kupewa huduma zote muhimu ikiwemo matibabu na chakula.
Watoto hao wamezaliwa kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Misheni ya Berega iliyopo Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro, Julai 21.
Mama wa watoto hao, Rebeca Mwendi Muya ni mkazi wa kitongoji cha Chaumbele mkoani Morogoro. Watoto hao ni wa jinsia ya kike na kiume na tayari madaktari wameshaanza kuwapatia matibabu ya kawaida.
Daktari aliyemfanyia upasuaji Rebeca, Alfred Chiponde amesema watoto hao wameungana tumboni hadi kifuani lakini kila mmoja ana mfumo wake wa hewa.
Comments