
Dk. Shein aliyasema hay leo Ikulu mjini Zanzbar wakati alipokutana na
uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na Bodi
ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati
Zanzibar (ZURA) na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar
(ZAWA).
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Mamlaka ya ZURA imeweza
kuleta matumaini makubwa katika kutatua changamoto kadhaa zilizokuwepo
hapo siku za nyuma katika suala zima la uhaba na upandishaji wa bei ya
mafuta kiholela uliokuwa ukitokea na kuleta usumbufu kwa wananchi.
Hivyo, aliitaka ZURA kuendelea na kasi na ari waliyonayo ya utendaji
wa kazi na kusisitiza haja ya kuiangakia kwa umakini sheria ya Mamlaka
hiyo kwani ina mambo mengi ya msingi yanayoigusa Bodi, Wizara na Jamii.
Dk. Shein alieleza kuwa kwa upande wa wananchi wanapaswa kuijua na
kuitambua ZURA na kazi zake ili kuweza kupeleka malalamiko yao hasa
katika suala zima la bei ya mafuta.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, alitoa
pongezi kwa ZURA na Bodi yake na kueleza haja ya kuangalia ujenzi wa
vituo vya kuuzia mafuta kwa kufuata sheria na taratibu za ZURA.
Waziri wa Wizara hiyo Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud
Talib, alipongeza mashirikiano yalipo kati ya Wizara na Bodi hiyo huku
akieleza changamoto iliyopo katika suala zima la ujenzi wa vituo vya
kuuzia mafuta ambao ujenzi wake umekuwa haufuati taratibu.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid
Yahya Mzee alieleza haja ya kutafutwa sehemu mbadala ya eneo la
kuhifadhia mafuta liliopo Mtoni ambalo kwa hivi sasa liko karibu sana na
maakazi ya wananchi.
Aidha, alisema kuwa tayari eneo la Mtoni miundombinu yake imechakaa
ambapo pia, meli za mafuta hivi sasa haziwezi tena kufika katika eneo
hilo sambamba na kueleza umuhimu wa kuwepo utaratibu wa kuuza maji kwa
magari ambayo hupeleka mahotelini kwani hiyo ni rasilimali ya Serikali.
Pia, Dk. Abdulhamid aliitaka ZURA kushirikiana na vyombo vya ulinzi katika kupambana na wauza mafuta ya magendo.
Nao uongozi wa ZURA ulieleza kuwa juhudi zimekuwa zikichukuliwa
katika kulitafutia ufumbuzi suala zima la miundombinu ya vituo vya
mafuta ambavyo vingi vimekuwa na vifaa vichakavu.
Wajumbe wa Bodi ya ZURA walimueleza Rais kuwa tokea kuanza kwa kazi
kwa ZURA suala la kuwepo kwa uhaba wa mafuta mara kwa mara limeondoka
sambamba na lile la wafanyabiashara kupandisha bei ya mafuta kiholela.
Walieleza kuwa kwa hivi sasa wameweza kujipanga vizuri na kupelekea
kuongeza mapato na kueleza mpango wao wa kutekeleza miradi mikubwa
ukiweo wa ujenzi wa ofisi zitakazojumuisha ofisi za Wizara ya Ardhi,
Maji, Nishati na Mazingira pamoja na ujenzi wa bandari kwa ajili ya
shughuli za mafuta na gesi huko Mangapwani.
Aidha, Mamlaka ya ZURA imeleeza mipango yake ya kutaka kubadilisha
mfumo wa uletaji mafuta hapa nchini ambapo mafuta yataletwa moja kwa
moja hapa Zanzibar hali ambayo itasaidia kushuka kwa bei ya mafuta na
kuweza kuwasaidia wananchi.
Pia, uongozi huo wa Mamlaka ya ZURA ulieleza kuwa tayari kumejitokeza
Makampuni kadhaa yanayotaka kushirikiana na Mamlaka hiyo katika ujenzi
wa Bandari huko Mangwapwani katika eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya
bandari pamoja na eneo kwa ajili ya mafuta na gesi.
Sambamba na hayo, ZURA ilieleza azma yake ya kulishughulikia suala
zima la maji na umeme ambalo limo katika majukumu yao kisheria ili
wananchi wapate kuzitumia vyema huduma hizo huku wakieleza mashirikiano
yao yaliopo kati yao na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji Tanzania
(EWURA).
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Mamlaka ya
Maji Zanzibar (ZAWA), uongozi wa Wizara husika pamoja na Bodi ya Mamlaka
hiyo na kutaka kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo hasa katika
suala zima la upatikanaji wa maji.
Dk. Shen pia, alieleza namna Serikali inavyoangalia haja ya
kuyahifadhi maji kwani maji yamekuwa yakipotea ovyo hasa mara baada ya
kumalizika kunyesha kwa mvua huku akiitaka ZAWA, Bodi, Uongozi wa Wizara
kuijua Sheria na kuifanyia kazi.
Nae Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, alieleza umuhimu wa
kutafuta ufumbuzi wa malalamiko ya upatikanaji wa maji katika maeneo
kadhaa ya wananchi hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA Mustafa Ali Garu alieleza jitihada
zinazochukuliwa na ZAWA ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi mikubwa
ukiwemo Mradi chini ya ufadhili wa Serikali ya China, Mradi wa ADB,
Serikali ya India ambao umo katika matayarisho, pamoja na Mradi kutoka
Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la misaada la JICA.
Alisema kuwa visima katika mradi wa ufadhili wa China unaenda vizuri
katika maeneo mbali mbali kama vile Donge, Chaani, Pangeni na maeneo
mengine ambayo tayari miudombinu ya maji imeshaanza kuwekwa.
ZAWA ilieleza kuwa mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa lakini hata
hivyo bado wanahitaji kujiimarisha katika kuongeza mapato hayo na
kueleza kuwa hilo linawezekana iwapo jitihada zaidi zitafanyika.
Alieleza kuwa hali ya maji yaliopo Zanzibar ni ya kutosha na kueleza
jinsi ilivyohuwika hasa katika kipindi kilichopita cha mvua za masika
ambapo maji yameweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Dk. Garu alieleza changamoto zilizopo ambazo ni pamoja na upotevu wa
maji huku akieleza kuwa hali ya miundombinu chakavu nayo hipo lakini
jitihada zimekuwa zikifanyika katika kuodoa tatizo hilo kupitia miradi
husika.
Nao Wajumbe wa Bodi ya ZAWA walieleza ponhezi zao kwa Rais kwa kuwepo
kwa mradi wa Ras-el kheiman ambao kukamilika kwake kutatatua changamoto
kubwa ya maji kwa upande wa Unguja na Pemba.
Walieleza changamoto zilizokuwepo ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa
miundombinu chakavu na kuongeza kuwa Mita za kawaida hazijaweza
kutosheleza ambapo bado kuna wateja wengi wanaohitaji huduma hiyo
kuipata.
Uongozi wa Wizara kwa upande wake ulieleza juhudi, malengo na
mikakati liyoiweka katika kuhakikisha changamoto ya sekta ya maji
inapatiwa ufumbuzi huku ikiitaka jamii kuitumia vyema rasilimali hiyo
iliyopo kwa kuihifadhi vyema pamoja na vianzio vyake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
chanzo: zanzibar24.
Comments