Aliyeua watu 17 wa familia moja kwa kuwakata mapanga atiwa mbaroni.

Mwanamume aliye fanya mauaji ya watu 17 wa familia moja wakazi wa Mugaranjabo wilaya ya Musoma mkoani Mara, kwa kuwakata mapanga wakiwa nyumbani kwao, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara.
 
Tukio hilo la mauaji ya watu 17 wa familia moja lilifanywa mwaka 2010  na Sura Bukaba Sura maarufu kwa jina la Phinias Yona au Epoda mwenye miaka 35, mkazi wa wilayani Butiama mkoani Mara ambaye amefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara mbele ya hakimu Richard Maganga.
 
Akisomewa mashitaka yake ya mauaji ya watu 17 , Mwendesha Mashitaka wa Polisi Jonas Kaijage, aliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa akiwa na wenzake wapatao 15, ambao wote wakazi wa wilayani humo, walitenda kosa hilo Februari 16 mwaka 2010 majira ya usiku katika eneo la Mugaranjabo, nje kidogo ya mji wa Musoma.
 
Kaijage alisema baada ya kutekeleza mauaji mtuhumiwa huyo alitoroka, na wenzake 15 walikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo  ambapo kati yao wanane walikwishafariki dunia wakiwa mahabusu.
 
Aidha Kaijage amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 18 mwaka huu, kwa kesi nyingine ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika eneo la Rwamulimi mjini Musoma.
 
Alisema katika tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha, mtuhumiwa huyo alivamia nyumbani kwa mwananchi mmoja na kuvunja nyumba kwa kutumia nondo na kufanikiwa kuiba Sh 500,000,ndipo polisi walifanikiwa kumkamata na kumtambua kuwa alishiriki katika tukio la mauaji ya watu hao 17 lililotokea mwaka 2010.
 
Baada ya kusomewa mashitaka yake mtuhumiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusilikiza kesi za mauaji na Hakimu Karimu Moshi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7 mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo na kuunganishwa na washitakiwa wengine waliosalia.
chanzo: zanzibar24.

Comments