Aliyegushi kufa Zanzibar ahukumiwa kwenda jela Uingereza.

Mahakama ya Birmingham imemhukumu Arafa Nassib (48) kwenda jela kwa miaka miwili na nusu baada ya kugundulika kuwa alidanganya kuwa amekufa ili kumuwezesha mwanawe Adil Kasim (18) kudai malipo ya bima ya maisha yenye thamani ya £136,000 ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 390 huku mwanawe Adili akihukumiwa kufanya kazi za kijamii kwa muda wa miezi 12.

Maafisa wa upelelezi wameeleza kuwa hawakukuta kaburi lake Zanzibar na waliambiwa kuwa anaishi Canada.


Awali kabla ya hukumu wawili hao walikubali kula njama na kuidanganya taasisi ya bima ya Scottish widows.

Aidha katika shauri hilo, Mahakama ilielezwa kwamba Arafa (48) alipunguza madeni yenye thamani ya £80,000 kabla ya kusafiri kwenda Zanzibar, ambapo ilisemekana amefariki katika ajali ya gari mwezi april mwaka jana.


Pia Mahakama hiyo ilielezwa kuwa Bi. Arafa ambaye aliingia nchini uingereza akitokea kenya 1998 kama mkimbizi, ana madeni na kampuni za fenicha za BrightHouse na PerfectHome.

Mwendesha mashtaka Jonathan Barker aliiambia mahakama hiyo kuwa Bi. Arafa alijiunga na bima ya maisha kwa jina la awali mnao mwaka 2013, huku akimuweka mwanawe huyo kama mrithi. Na kama wangefanikiwa basi wangelipwa £136,000, alisema Barker

Katika madai hayo ya uongo ilielezwa kuwa Bi. Arafa alifariki kutokana na majeraha ya kichwani na kuambatanishwa cheti cha kifo chenye tarehe 14 April.

Baada ya hapo wapelelezi wa shirika la Bima walisafiri kuja Zanzibar na waligundua kuwa daktari anaetajwa kumtibu  Bi. Arafa hakuwa kazini siku iliyotajwa kufariki kwake.

Bi. Arafa alirudi Uingereza kwa ndege ya Emirates na alisafiri kwenda Canada baada ya kuzungumza na simu na mwanawe akiwa Uingereza.

Mwendesha mashtaka huyo alimaliza kwa kusema “Bi. Arafa ndie kiongozi wa njama hizi na alimhusisha mwanawe”
 chanzo:zanzibar24.

Comments