Chama
cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimemuomba Rais John Magufuli
kuachia vyama vya siasa vya upinzani kufanya shughuli za kisiasa kwa
kuwa ni takwa la kisheria.
Kauli
hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Taifa wa chama
hicho, Doyo Doyo aliyesema hali ya kisiasa nchini si nzuri na kwamba
Serikali kwa kuendelea kuzuia shughuli za kisiasa ni tishio kwa vyama
kama ADC akisema huenda vikafa.
“Hali
ya kisiasa sio nzuri sana, kuna hali ya kutopata uhuru wa kufanya siasa
hasa katika upande wa vyama vya upinzani katika nchi yetu. Kuzuiwa
kufanya mikutano ya kisiasa, makongamano na kadhalika, hii inaua vyama
vya siasa,”alisema na kuongeza:
“ADC inamuomba Rais John Magufuli atuachie tufanye mikutano kwani jambo hili ni takwa la kisheria.”
Akizungumzia
usalama nchini alisema hawaridhishwi na taarifa za mauaji yanayoendelea
Kibiti mkoani Pwani akisema yanatia doa Taifa, ambapo aliiomba Serikali
kujipanga upya na kuweka mkakati madhubuti ya kukabiliana na wahalifu.
Kuhusu
migogoro ndani ya vyama vya siasa Doyo alisema ADC kinashangazwa na
mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) kushindwa kupatiwa ufumbuzi wa
haraka hali inayofanya wanachama wake kuanza kukata tamaa.
Alisema
ADC inachukizwa na hali hiyo kwani kuendelea kwa mgogoro huo kwa muda
mrefu ni kunadhoofisha afya ya upinzani katika macho ya Watanzania.
“Nawaomba Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba wakae pamoja ili kumaliza tofauti zao,” alisema Doyo.
Aidha,
alieleza kushtushwa kwa ADC na matamko mbalimbali ya viongozi wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuingilia mgogoro huo wa CUF.
Doyo
aliwashauri Chadema kuacha mara moja kuingilia mgogoro usiowahusu
akidai kitendo hicho cha kuingilia mgogoro huo usiowahusu ni mkakati wa
kisiasa wa kujitengenezea hati miliki ya kisiasa nchini, lakini pia
kinaweza kuhatarisha amani.
Hata
hivyo, Doyo alisema alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake
anazofanya kuzuia rasilimali za nchi hasa kwa kitendo cha kuwasilisha
miswada kwa hati ya dharura bungeni ili kufanyiwa marekebisho ya sheria.
chanzo:Mpekuziblog.
Comments