Waganga tiba asili nchini waonywa kuhusu himofilia.

WAGANGA wa tiba asili na mbadala nchini, wameshauriwa kuwapa rufaa wagonjwa wa Himofilia wanaofika katika vituo vyao kwa tiba ili kuepusha madhara zaidi kwa waathirika wa ugonjwa huo.

Ushauri huo ulitolewa jana na Rais wa Chama cha Watu wenye Himofilia Tanzania, Richard Minja wakati akitoa hotuba ya makaribisho katika semina kwa waganga wa tiba asili na mbadala wa jijini Dar es Salaam iliyofanyika jijini humo. 


Alisema wagonjwa wengi wa himofilia wamekosa tiba stahili na kusababisha athari kubwa hata wengine kufa kutokana na kutopewa maelekezo mazuri na waganga wa tiba asili na mbadala wanapofika kwao kupata matibabu.

“Tumewaita waganga wa tiba asili kupata semina kuhusu himofilia ili waufahamu vizuri ugonjwa huu na wasaidie kuwapa rufaa wagonjwa maana ugonjwa huu ni wa kisayansi na tiba stahiki inapatikana hospitalini,” alisema Minja. 

Alisema semina hiyo kwa waganga hao imeanzia Dar es Salaam na itafikishwa nchini kote hasa vijijini ili kuwasaidia watoa tiba hao kuuelewa ugonjwa huo na kushirikiana na vituo vya afya na hospitali kuwaelekeza wagonjwa kupata tiba inayotakiwa kisayansi.

Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya damu na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Damu Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Stella Rwezaula, alisema wameelekeza semina kwa waganga wa tiba asili na mbadala kwa kuwa Watanzania wengi wanakwenda kwao kuhitaji msaada. 

Akielezea hali ya ugonjwa, Dk Rwezaula alisema kwa sasa nchini wamesajili wagonjwa 110 pekee wa himofilia lakini zaidi ya Watanzania 5,400 wanaishi na ugonjwa huo na asilimia 97 hawajitambui kama wanao.

Aliwataka wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya ili kutambua kama una ugonjwa huo au mwingine ili kuanza tiba na ushauri zaidi. 

Dk Rwezaula alisema ugonjwa huo unatokana na mtoto kuzaliwa akiwa amepungukiwa na protini ya kugandisha damu ikiwa ataumia. Alisema kutokana na upungufu huo, muathirika anapoumia, kupata ajali au mjamzito wakati wa kujifungua hutoka damu nyingi na wakati mwingine kusababisha vifo.

Alisema ingawa bado nchini utafiti wa kina haujafanywa kuhusu ugonjwa huo, kwa sasa muathirika ataishi nao maisha lakini atapata tiba ya kumpa ahueni kwa njia ya dawa (factor namba 8 na 9) na huchomwa kwa njia ya sindano. 

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili Tanzania (Shivyatiata), Othuman Shem, aliwashukuru waandaaji wa semina hiyo kwa kuwakumbuka waganga wa tiba asili na mbadala kupata semina hiyo kuwezesha kuwapa rufaa wagonjwa wenye tatizo hilo pindi watakapowafikia.

“Semina ni nzuri maana tumejua kuwa ni ugonjwa wa kisayansi wala si mapepo au majini, hii itasaidia maana zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanakuja kwetu kwa tiba asili, tukiuelewa huu ugonjwa, mtu akija ni rahisi kumshauri aende hospitali,” alisema Shem. 

Alishauri semina hiyo ifanyike nchi nzima ili waganga wengi wa tiba asili na mbadala waipate kunusuru maisha ya Watanzania wenye himofilia.
chanzo:Habarileo.

Comments