Tanzania inazalisha tani 260,000 za korosho kwa mwaka na sasa ina
viwanda 12 vya ubanguaji.
Akizungumza Dar es Salaam jana juu ya umuhimu
wa kuacha utaratibu wa kusafirisha korosho ghafi zinazoyanufaisha
mataifa mengine,
Mtafiti Kiongozi wa Programu ya Korosho Barani Afrika
ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Profesa Peter
Masawe, amesema kiasi kikubwa cha thamani ya korosho kinapotea kwa
kukosa umakini.
“Wabanguaji wa Tanzania wanachukua korosho karanga tu huku wakiacha
kiasi kikubwa cha zao hilo ikiwemo maganda na mabibo ambayo yana thamani
kubwa. Tutafute namna ya kuyaongezea thamani maganda na mabibo badala
ya kutupa,” alisema.
Profesa Masawe alitolea mfano mataifa yanayonufaika na korosho za
Tanzania ikiwemo India: “Tujiulize kwa nini mataifa ya India, China na
Vietnam ndio walionunua korosho nyingi katika msimu uliopita kuliko
wabanguaji wa ndani mbali ya kilo moja kufikia Sh 4,000 tena bila kujali
gharama ya kusafirisha na kuhifadhi kwenye maghala wakifika kwao; maana
yake wanapata faida kubwa.
“India, kwa mfano, wakibangua korosho ikitoka karanga wanaiuza kama
chakula, vipande vya korosho wanatengenezea siagi, pasta na poda.
“Kwenye maganda, wanatoa CNSL (Cashew Nut Shell Liquid) ambayo uzito
wake inakua sawa sawa na korosho iliyotoka; yaani ikiwa ulipobangua
ulipata kilo 10 ya korosho basi utapata kilo 10 ya CNSL ambayo inatumika
kutengenezea brake linings, vipodozi, viuatilifu vya kuua mchwa na
kilainishi katika mashine za ndege,” alisema Profesa Masawe.
Kwa upande wa mabibo, mtafiti huyo aliyebobea kwenye korosho alisema,
juisi ya mabibo ina vitamin C mara 10 zaidi ya juisi ya nanasi na mara
tano zaidi ya juisi ya machungwa, lakini pia mabibo yanatumika
kutengeneza mvinyo na pombe kali aina ya Nipa. “Tukianzisha viwanda
vitatu tutakuwa tumeiunga mkono serikali yetu katika azma ya kutufikisha
katika uchumi wa viwanda.
Tujiulize ikiwa kiwanda kimoja kina uwezo wa kubangua tani 10,000
sisi tunazalisha tani zaidi ya 260,000 kwa mwaka na nina hakika msimu
ujao tunaweza kufikia tani 300,000. “Maana yake tukiwa na viwanda zaidi
ya 20 vinavyobangua tani 10,000 kila kimoja na kila kiwanda kikiwa na
uwezo wa kutoa ajira zaidi ya 8,000, hizo ni ajira 80,000. “Kumbuka
viwanda vingi havipo mjini, vipo maeneo zinapozalishwa korosho huko
vijijini, kwanza tutapunguza msongamano mjini lakini pia tutaimarisha
elimu, afya na miundombinu vijijini,” alisema.
Takwimu zinaonesha korosho ni zao linalokua kwa kasi katika ukanda
huu wa kusini mwa jangwa la Sahara na msimu uliopita liliongoza kwa
mauzo. Hata hivyo, Tanzania ina viwanda 12 vya kubangua korosho lakini
changamoto ya kuuza korosho ghafi nje ya nchi haijapatiwa ufumbuzi.
chanzo:Habarileo.
Comments