Uzinduzi huo uliofanyika Dar es Salaam jana, utawawezesha watanzania kujiunga na kupata utaalamu na vyeti vya VETA kwa gharama nafuu Kozi hizo mpya zilizozinduliwa ni huduma ya chakula na mbinu za kuhudumia wateja, matengenezo ya kompyuta, umeme wa viwandani, ufundi bomba wa majumbani na umeme wa magari.
Uzinduzi wa kozi hizo ni mfululizo wa juhudi za mamlaka ya Veta, kufikia vijana wengi katika kazi zao bila kuwaharibia ajira zao. Tangu kuzinduliwa kwa mfumo huu wa mafunzo kwa njia ya mtandao kupitia programu ya VSOMO Juni 2016, vijana zaidi ya 30,000 tayari wamepakua programu ya VSOMO, 8000 wamejiandikisha na kati yao 50 wanasoma kozi mbalimbali zilizopo pia wapo waliomaliza na kupata vyeti vya VETA.
Mfumo huo ulipoanza, kozi zilizotolewa ni pamoja na ufundi umeme wa majumbani, ufundi pikipiki, ufundi wa simu za mkononi, ufundi Aluminium, utaalamu wa masuala ya urembo pamoja na ufundi wa kuchomea vyuma.
Akizungumza wakati wa kuzindua na kutangaza kozi hizo jana, Mkuu wa Chuo cha Veta Kipawa, Lucius Luteganya alisema: “Mafunzo ya ufundi kwa njia ya mtandao ya VSOMO yametuwezesha kuongeza wigo na kuwafikia watanzania wengi nchini.
“ Alisema anaamini bado iko fursa ya kuongeza wigo zaidi na kuongeza idadi ya vijana wenye ueledi ili kwenda sambamba na ajenda ya serikali ya Awamu ya Tano ya uchumi wa viwanda, kwa kupata nguvu kazi yenye taaluma muhimu katika kuendesha uchumu wa nchi.
“Tunaamini kozi hizi mpya, zitawavutia vijana wengi kujiandikisha, kusoma na kupata ujuzi zaidi,” alisema Luteganya. Akifafanua, Luteganya alisema ili kupata mafunzo ya VSOMO kupitia Airtel, kijana anatakiwa kupakua application katika google play store, na kujisajili na kisha kuchagua kozi inayokidhi mahitaji yake.
Wale watakaomaliza masomo yao ya nadharia kupitia VSOMO, watafanya mtihani ili kufaulu na kujiunga na mafunzo ya vitendo katika vituo vya VETA vilivyopo nchi nzima. Vyeti vya kuhitimu mafunzo vitatolewa kwa wale watakaofaulu mafunzo katika hatua zote mbili ya nadharia na vitendo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano alisema taasisi yake inajisikia furaha kuongeza kozi nyingi zaidi katika mfumo huo wa masomo kwa njia ya mtandao wa VSOMO.
“Tunapenda kuwapongeza wote waliojiunga na kumaliza kozi zao na kuhimiza wote ambao hawajapakua application ya VSOMO kufanya hivyo kwa kujiandikisha katika mojawapo ya kozi 12 zinazopatikana katika application ya VSOMO kwa gharama nafuu ya shilingi 120,000 tu na kulipia kwa njia ya Airtel Money”, alisema Singano.
chanzo:Habarileo.
Comments