SHERIA ya uharibifu wa mazao yawamurika na Masheha : Jaji Mshibe.

Sheria ijayo ya kudhibiti uharibifu wa mazao, itawabana  masheha wenye tabia ya kutoa vibali kwa wafanyabiashara, wanaosafirisha mazao machanga au yalioivishwa kwa moto ikiwemo ndizi.

hayo yameelezwa na MWENYEKITI  wa Tume ya kurekebisha sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakari, kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na masheha wa mkoa wa kaskazini Pemba pamoja na wadau wengine alipokuwa akifungua mkutano wa uwasilishaji wa rasimu za awali za sheria  ya uharibifu wa mazao, sheria ya usajili wa nyaraka na urithi wa ardhi endelevu mkoani humo.

Alisema kwa sasa sheria hiyo inaendelea kufanyiwa mapitio na tume yake kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali  na ndani ya sheria hiyo vitakuwemo vifungu vinavyowagusa viongozi hao wa shehia iwapo watatoa vibali kiholela.

Alisema wapo wafanyabiashara wanao yaharibu mazao kwa makusudi  kwa kuyachuma machanga au kuyaivishia kwa moto huku masheha wakishuhudia na kuvifumbia macho vitendo hivyo jambo ambalo si sahihi na katika sheria  ijayo suala hilo litahesabika kama kosa.

Aidha Mwenyekiti huyo wa tume ya kurekebisha sheria, alisema hata masheha kama wakijaribu kuwapa vibali vya kusafirishia wafanyabiashara wenye tabia hiyo, nao sheria inawamulika hivyo lazima wajitenge na jambo hilo.


“Sheria hii ambayo ni kongwe na sasa inafanyiwa marekebisho, haitowagusa tu waharibifu wa mazao kama vile wafanyabiashara wanaoingiza au kutoa nje ya Zanzibar mazao, hata masheha wakitoa vibali kwa  waharibifu nao watawajibika”,alifafanua.

Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo, aliitaja jamii kuendelea kujenga utamaduni wa kusajili nyaraka zao pamoja na ardhi ili ziwe na thamani kisheria.

Mapema Katibu wa Tume hiyo Asma Hamid Jidawi, alisema sheria ya usajili wa ardhi endelevu, unalengo pia la kuondoa migogoro kwenye ardhi za matumizi endelevu kama vile viwanja wa michezo, misikiti na makanisa.

Baadhi ya masheha wa mkoa wa kaskazini Pemba, walisema kama sheria hiyo itatekelezwa ipasavyo baada ya kupitishwa yaweza kuwa ni mwarubani wa mazao kununuliwa yakiwa na uasili wake sokoni.

Sheha wa shehia Micheweni Dawa Juma Mshindo alisema Zanzibar inazosheria nyingi na mzuri, ingawa changamoto huja kwenye utekelezaji wake.

Akiswalisha mswada wa sheria ya usajili wa nyaraka mwanasheria kutoka tume hiyo Mwita Khamis Haji, alisema sheria hiyo imeeleza aina mbili za nyaraka zikiwemo za lazima na nyengine ambazo ni hiari.

“Nyaraka ya nyumba unayoishi au wa kiwanja cha nyumba hizi ni lazima, ingawa zipo nyengine kama vile mikataba ya kijamii hizi hulazimiki, ingawa faidi yake ukizisajili zipo”,alisema.

Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake jaji Mshibe Ali Bakar imeshazifanyia marekebisho sheria 17 ikiwemo sheria ya ushahidi, sheria ya wanyama, vileo na sheria ya usafirishaji baharini, na kwa sasa wanaendelea na sheria za uharibifu wa mazao, nyaraka na ardhi endelevu.
chanzo: zanzibar24.

Comments