Serikali bado haijui katikati ya Tanzania ni wapi.

Serikali imepata kigugumizi cha wapi ni katikati ya Tanzania na bado ipo katika mkakati wa kutafuta eneo hilo.
Awali Watanzania waliamini kuwa katikati ya nchi ni Dodoma lakini baadaye wanasiasa wakongwe walieleza katikati ya Tanzania ni eneo la Mhalala lililoko wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Akizungumza bungeni leo (Ijumaa Juni 30) Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amekanusha kuwa hakuna taarifa rasmi za kitaaluma zinazoonyesha kwamba kijiji cha Chisinjisa kuwa ndiyo katikati ya nchi (Center point).

Katika swali la msingi Mbunge wa Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka alitaka kujua ni lini serikali italitambua rasmi eneo hilo na kulitangaza katika gazeti la Serikali.
“Je Serikali haioni umuhimu wa kuendeleza na kulitangaza eneo hilo ili kuvutia utalii wa ndani na nje ya nchi kama chanzo cha mapato,” alihoji Mtuka.
Naibu Waziri amejibu akisema wizara kwa kupitia idara ya upimaji na ramani inakusudia kufanya utafiti wa kina kwa kutumia elimu ya geomatika (geomatics) ili kubaini eneo rasmi ambalo alama ya katikati ya Tanzania (center point) inapatikana.
Amesema baada ya utafiti huo kukamilika, eneo la katikati ya nchi litatangazwa katika gazeti la Serikali.
“Aidha, mamlaka zinazohusika na masuala ya utalii zitaendeleza eneo husika ili kuvutia utalii wa ndani na nje ya nchi kama zinavyofanya nchi nyingine duniani na kuongeza mapato ya Serikali,” amesema Mabula.
Kuhusu kutoa tamko la kutuma wataalam kuanza kulifanyia kazi eneo hilo, alisema itakuwa ni ngumu kwa sasa kwani bado mchakato wake unaendelea kwa utaratibu ambao wizara imejiwekea.
chanzo:Mwananchi.

Comments