Pinda aisifu Repoa katika utafiti.



Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda 
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema hatua mbalimbali za mafanikio ya kiuchumi katika serikali ya awamu ya tatu na ya nne yametokana na utumiaji wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Repoa.
Kauli hiyo ameitoa leo (Ijumaa) jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kitabu cha Taasisi hiyo kiitwacho ‘Research and Policy Nexus: Perspective from twenty years of Policy research in Tanzania.’

Pinda aliyemwakilisha Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete amesema utekelezaji wa mradi wa kupunguza na kuondoa umaskini Tanzania (MKUKUTA) awamu ya 1 na 2 ulipata mchango mkubwa kutokana na tafiti mbalimbali za Repoa.
“Repoa imekuwa ikitafiti mambo yanayogusa wananchi kila siku, yanaweza kuwa kijamii, kiteknolojia, kiuchumi na mengi, ukitazama dira ya maendeleo, Mkukuta yenyewe, mpango wa miaka 15 umeandaliwa katika awamu ya nne na ulitokana na tafiti za watalaam hawa,” amesema.
Kwa mujibu wa Repoa, kitabu hicho kinalenga kuzungumzia umuhimu wa uhusiano kati ya sera na tafiti katika mafanikio na siku zijazo.
Ofisa Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari, amesema katika kipindi cha miaka 20, taasisi hiyo imeshuhudia mageuzi makubwa ya kisera.
“Sera hizo ziliandaa mazingira ya muundo wa sasa wa kiuchumi na kijamii ili kuonyesha mwelekeo wa taifa katika hatua za kuchukua,” amesema.
"Utungaji wa sera nchini umebadilika sana katika miongo miwili iliyopita, katika michakato ya utungaji sera tangu wakati huo, unatupatia uhalali (Repoa) kutoa simulizi ya baadhi ya shughuli za Repoa na washirika wake sambamba na taasisi washirika, kwa namna tulivyoshiriki kutoa mwelekeo wa sera nchini,"amesema Dk Mmari.
chanzo:Mwananchi.

Comments