
Tahadhari hiyo imetolewa na Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni CCM
Taifa, Nd. Pereira Ame Silima katika mwendelezo wa ziara yake huko Mkoa
wa Kusini kichama Unguja, alisema mtu aliyewania nafasi ya uongozi
ndani ya chama hicho hana haki ya kujadili na kuchuja fomu za wagombea
wenzake kwani kufanya hivyo ni kinyume na Katiba ya Chama hicho.
Alisisitiza kwamba katika zoezi hilo ni lazima kila kiongozi asimamie
taratibu za uchaguzi ili kuepuka malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
“ Kuna baadhi ya matawi kumetokea changamoto za baadhi ya wagombea
kujadili na kupitisha fomu za wagombea wenzao jambo ambalo ni kinyume na
taratibu za Kikatiba hivyo hatuwezi kuvumilia vitendo hivyo ni bora
uchaguzi urejewe katika maeneo yaliyoripotiwa ukiukaji wa miongozo
yetu”, alisema Nd. Pereira.
Nd. Silima alisema dhamira ya chama hicho ni kuhakikisha chaguzi zote
zitakazofanyika ndani ya chama na jumuiya kuhakikisha wanapatikana
viongozi bora waliopatikana kwa mujibu wa matakwa ya Kikatiba na sio
watu binafsi.
Katibu huyo aliweka wazi msimamo wake kwamba atapambana vikali na
baadhi ya watu waliopandikizwa katika uchaguzi huo ili wapange safu na
makundi ya viongozi wanaowataka wao kwa baadhi ya ngazi za uongozi .
Aidha aliwasihi viongozi hao kumpa ushirikiano wakati wa utekelezaji
wa majukumu ya kiutendaji hasa katika jukumu la kufanikisha uchaguzi
unaoendelea na kuhakikisha unakamilika kwa kiwango kilichokusudiwa.
“ Lengo la ziara yangu ni kujitambulisha kwenu kwani toka
nilipoteuliwa sijawahi kuja kwenu kubadilishana mawazo pia naomba
ushirikiano katika Idara yangu ya organazesheni ambayo jukumu lake la
msingi ni kusimamia shughuli zote za chaguzi za chama na dola pamoja na
masuala ya takwimu za wanachama.”, alisema Silima.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya uchaguzi wa chama hicho kwa
ngazi za Matawi, Kaimu Katibu wa Wilaya ya Kusini Kichama Unguja, Hafidh
Hassan Mkadam alieleza kuwa changamoto iliyojitokeza katika zoezi hilo
ni baadhi ya Viongozi wa ngazi husika kufanya uteuzi bila ya kuzingatia
kanuni ya uchaguzi na katiba ya CCM, hali iliyopelekea baadhi ya matawi
kurejea zozezi hilo.
chanzo:zanzibar24.
Comments