Mwenyekiti
wa CHADEMA na Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Freeman
Mbowe ameonesha kusikitishwa na mauaji ya raia wasiokuwa na hatia
yanayoendelea katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji.
Mbowe
alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia msimamo wa CHADEMA juu ya
mauaji hayo ambapo alisema chama hicho kinapingana na kinachotokea Mkoa
wa Pwani.
“Kinachoendelea Mkuranga, Kibiti na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani ni kitu kibaya. Hatuungi mkono mauaji ya raia na viongozi.
"Hilo
naomba niliweke wazi, sisi kama chama hatuungi mkono mauaji ya viongozi
bila kujali wanatoka chama gani au bila kujali wanatoka Serikali ipi au
wana wajibu gani wala raia yeyote wa nchi yetu. Hatuungi mkono na
tunalaani sana mauaji yanayoendelea.”
Aidha,
alisema wanasikitika na namna Serikali inavyolichukulia suala hilo
akiwataka viongozi wa kisiasa kuviachia vyombo vya Ulinzi na Usalama
vifanye kazi yake.
“Tunasikitika na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyoshughulika na jambo hili.
"Kauli
za viongozi wetu mbalimbali za majigambo zinaonekana kuwachochea wauaji
kwa sababu linapotoka tamko lolote la majigambo anakufa mtu usiku ama
anakufa mtu kesho yake.
"Viongozi
wetu wa kisiasa waachie vyombo vya Ulinzi na Usalama vifanya kazi.
Matamko mengi yanatolewa na viongozi wetu wa kisiasa. Hatuna hakika ni
nini kinaendelea.”
Katika
kutafuta suluhisho zaidi juu ya tatizo la mauaji ya Pwani, Mbowe
alivitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutumia ujuzi wa ziada
kukabiliana na wauaji ikiwa pia kuwashirikisha watu mbalimbali na
taasisi mbalimbili.
“Tunataka
Majeshi yetu na vyombo vyetu vya Ulinzi na Ulasama vitumie weledi wa
ziada. Sio kila wakati nguvu tu inaweza ikasaidia. Busara nyingine zote
zitumike; Wazee watumike, Vyombo vya Serikali vitumike, Viongozi wa
Kidini watumike.”
chanzo:Mpekuziblog.
Comments