Mawaziri wakuu wastaafu Dk Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba hawakutoa neno lolote jana katika mjadala wa Kongamano la Tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere licha ya mwongozaji wa mjadala huo ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala kuwapatia nafasi ya kuchangia.
Wakati wa mjadala huo, watu mbalimbali walitoa mitazamo yao kumuuliza maswali mwanakigoda wa mwaka ambaye ni mwanasiasa na mwanadiplomasia kutoka Senegal, Profesa Abdoulaye Bathily, lakini mwongozaji alipotaka wastaafu hao wapewe kipaza sauti ili kuchangia walitikisa vichwa vyao, wakiashiria kuwa hawakuwa wakihitaji kuzungumza.
Alianza kutajwa Dk Salim kisha Jaji Warioba, lakini hawakuwa tayari kuzungumza.
Baada ya kumalizika kwa mjadala huo na kufuatiwa na mapumziko ya dakika 30, waandishi wa habari walimfuata Jaji Warioba kwa ajili ya mahojiano na kuahidi kwamba angezungumza baada ya mapumziko hayo lakini baada ya muda alipanda gari lake na kuondoka.
Katika kongamano hilo, wanasiasa barani Afrika walitupiwa lawama kwa kushindwa kufanya mageuzi ya kimtazamo ambayo yanaweza kuendeleza nchi zao na bara zima kwa ujumla badala yake wanakumbatia wahisani ambao mambo mengi wanayafanya kwa masilahi ya mataifa yao.
Mada kuu katika Kongamano hilo la Tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere linalofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Nkrumah uliopo UDSM ni “Nafasi ya wanasiasa katika kuinuka na kuanguka kwa maendeleo ya Bara la Afrika.”
Akizungumza suala hilo, Profesa Bathily alisema Afrika imekombolewa takriban miongo minne sasa, lakini bado inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo magonjwa, ukosefu wa ajira na ukimbizi ambao unasababishwa na migogoro katika baadhi ya mataifa.
“Afrika imekosa viongozi wenye mtazamo chanya kwa ajili maendeleo ya Afrika ya leo na baadaye. Hayo yote ni kwa sababu viongozi waasisi hawaenziwi kwa matendo yao na maandiko waliyoyaacha, wao waliungwa mkono na kufanikiwa katika ukombozi kwa kuwa walikuwa na mtazamo wa kuona ni kitu gani umma unataka,” alisema Profesa Bathily.
Alisema Afrika haiwezi kuendelea bila kuungana na kuwa na nguvu moja, kuangalia ni mambo gani yana manufaa ya muda mrefu kwa Waafrika na si kila kiongozi kuangalia masilahi ya nchi yake pekee. Waafrika wanapaswa kuwa ndiyo washiriki wakuu wa kujenga uchumi wao.
“Afrika ya sasa ni utengano, kila nchi ina wabia wake, lakini ukweli ni kwamba wabia kutoka nje hawawezi kuwaletea maendeleo Waafrika, ndiyo maana Afrika inaendelea kuwa bara la kuzalisha malighafi na bidhaa zinazalishwa kwingine. Hata mashamba yanayolimwa na wawekezaji wa mataifa mengine ni kwa ajili ya manufaa yao na si chakula kwa Waafrika,” alisema Profesa Bathily.
Alisema nchi za bara la Asia zimeendelea kutokana na viwanda, biashara na kilimo ambavyo vimetoa ajira kwa raia wake, lakini Afrika hata ujenzi wa miundombinu yoyote wataalamu wote wanatoka katika mataifa ya Magharibi badala ya kuendeleza watu wa ndani ili kuwa na Taifa la watu wenye ujuzi.
Profesa Ophelia Mascarenhas aliyeshiriki kongamano hilo, aliisema mjadala katika mada hiyo ulikuwa ni mzuri lakini jambo la kutaka Afrika kuungana lina ugumu wake kwa sababu kila nchi ina mtazamo wake na matatizo yake.
“Kwa mfano, leo kuna ambao wanataka kuendelea kupokea msaada kutoka kwa wahisani wao, kuna ambao wanafanya mapinduzi ya viwanda. Kila kiongozi wa nchi atakuwa na vipaumbele vyake ambavyo kwa upande wake ataona vina masilahi kwa taifa lake,” alisema Mascarenhas.
Awali, katika ufunguzi wa kongamano hilo, Profesa Mukandala alisema wasomi, viongozi mbalimbali na wasanii wa kizazi kipya watapata nafasi ya kutoa mawazo yao juu ya mada husika.
Comments