IOM: Wanaofanya magendo ya wahajiri wanapata dola bilioni 35 kwa mwaka.

Shirika la Wahajiri Duniani IOM limesema watu wanaofanya biashara haramu ya magendo ya wahajiri wanatengeneza faida ya dola bilioni 35 za Marekani kila mwaka.

Mkuu wa IOM, William Lacy Swing ameliambia shirika la habai Reuters kuwa, kuongezeka idadi ya watu wanaokimbia nchi za Afrika kutokana na vita, umaskini na ukosefu wa ajira kumesababisha kushamiri biashara hiyo haramu ambapo wahajiri wanaotaka kwenda bara Ulaya kupitia bahari ya Mediterania hutozwa ada.

Amesema watu waliopoteza maisha tangu mwaka uanze hadi sasa wakivuka moja ya maeneo hatari zaidi baharini kwa lengo la kukimbia umasikini na vita barani Afrika na Mashariki ya Kati imepindukia 1,700 na kwamba idadi ya wahajiri ambao miili yao imezama katika bahari ya Mediterania na kufukiwa na mchanga wa Sahara haijulikani.
Amesema idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na takwimu za mwaka jana ambapo zaidi ya wahajiri 5,000 hususan wa Kiafrika walipoteza maisha kwa kuzama katika bahari ya Mediterania wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya, huku mwaka juzi 2015 ukishuhudia wahajiri 3,700 wakifa maji katika safari hizo zenye hatari kubwa sana.
Mkuu wa Shirika la Wahajiri Duniani ameongeza kuwa, nchi za Ulaya zinafaa kuunda sera ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa wahajiri lakini amesisitiza kuwa binafsi haoni jambo likifanyika hivi karibuni.
chanzo:parstoday.

Comments