Halmashauri zinazotaka nyumba NHC zashauriwa kujiandaa.

HALMASHAURI zinazotaka kujengewa makazi na Shirika la Nyumba Taifa (NHC) zinatakiwa kutenga maeneo, kulipa fidia na kuweka miundombinu.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanislaus Nyongo (CCM). Nyongoa alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kulialika NHC kujenga nyumba katika mkoa mzima wa Simiyu.

Mabula alisema hadi sasa halmashauri mbili za Busega na Bariadi ndizo zimetenga maeneo kwa ajili ya NHC kujenga nyumba, na zinazobaki zinatakiwa kutenga maeneo, kuwalipa fidia wananchi wenye maeneo na kuweka miundombinu ili kujenga nyumba hizo. 


Alisema halmashauri hizo zinatakiwa kuwa na uhakika wa matumizi ya nyumba hizo, kwani kuna halmashauri 30 ambazo zimejengwa nyumba na NHC na hazitumiki.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga (CCM) aliyetaka kujua ni lini ahadi ya Rais ya wakati wa Kampeni mwaka 2015 itatekelezwa ya kujenga za watumishi katika wilaya ya Itilima, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema katika mwaka 2017/18, serikali imetenga Sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za watumishi.

“Katika mwaka wa fedha 2016/17, serikali ilitenga Sh milioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za watumishi,” alisema. Aidha, serikali imetoa Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na ujenzi wake unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
chanzo:Habarileo.

Comments