Akikabidhi nyaraka za boti hiyo kwa Mkuu wa Wilaya Kigoma, Samson
Anga Meneja wa mradi wa uhifadhi mazingira na kuinua kipato kwa jamii wa
BTC, Mayuma Cheyo alisema kuwa boti iliyogharimu kiasi cha shilingi
milioni 19.5 itatumika kwa ajili ya shughuli za mradi katika eneo la
mwambao wa Kaskazini wa ziwa Tanganyika.
Cheyo alisema katika utekelezaji wake boti hiyo itatumika kwa ajili
ya kusafirisha watu wanaohusika na utekelezaji wa mradi, kufanya doria
kuzuia uvuvi haramu na kulinda mazao ya samaki ambayo yamekuwa
yakiharibiwa kwa kasi.
Akizungumza baada ya kupokea boti hiyo Mkuu wa
wilaya Kigoma, Samson Anga ametaka boti hiyo kutumiwa kwa shughuli
zilizopangwa ili kuleta tija katika utekelezaji wa mradi huo.
Pamoja na hilo alisema boti hiyo itatumika pia kwa shughuli nyingine
za maendeleo za utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwani kumekuwa na
shida kufikia maeneo ya mwambao wa ziwa kutokana na kutokuwepo kwa
nyenzo za usafiri kama hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kigoma,
Hanji Godigodi alisema kuwa pamoja na kudhibiti uvuvi haramu na
uharibifu wa mazingira katika vijijini vya mwambao wa ziwa Tanganyika
lakini pia uwepo wa boti hiyo itasaidia katika ukusanyaji mapato wa
leseni za uvuvi na mapato mbalimbali ya halmashauri.
Godigodi alisema kabla ya kupatikana kwa boti hiyo uvuvi haramu
ulikuwa unafanyika kwa kiasi kikubwa kutokana na watendaji wa
halmashauri kushindwa kuwafikia wavuvi wanaovua kwa kutumia nyavu
haramu.
Alisema walikuwa wakiwakimbia na kukimbilia kwenye kina kirefu
cha maji, jambo ambalo halikuwa na ufanisi kwenye kudhibiti uvuvi haramu
ambapo sasa boti hiyo itasaidia kukomesha uvuvi haramu.
Wenyeviti wa kamati za ulinzi za rasilimali za ziwa Tanganyika (BMU),
Meko Mwangi kutoka Kijiji cha Mtanga na Mwema Hussein kutoka Kijiji cha
Kigalye wamesema kuwa ulinzi waliokuwa wakiufanya bila kuwepo kwa
nyenzo za kufanyia kazi ilikuwa kazi ngumu kwao na kwamba sasa udhibiti
wa uvuvi haramu utafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
chanzo:Habarileo.
Comments