
Naibu Waziri Mkuu Mstaafu ambae pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha
Nchini Mauritius Dr. Ramakrishna Sithanen alieleza hayo katika
mazungumzo ya pamoja na Watendaji Wakuu wa Sekta za Viwanda, Biashara,
Utalii, Uwekezaji na Mipango chini ya Uwenyekiti wa Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Dr. Ramakrishna Sithanen ambae ni Mtaalamu na pia Mshauri Muelekezi
katika Sekta ya Viwanda, Utalii, Biashara, Mipango na Uwekezaji alisema
changamoto zote zinazoibuka katika harakati za Maendeleo hupata ufumbuzi
wa haraka wa kukabiliana nazo katika njia ya uwajibikaji wa pamoja.
Alitanabahisha wazi kwamba ukuaji wa uchumi lazima uende sambamba na
ujenzi wa miundombinu imara itakayosaidia pia kudhibiti ongezeko la
idadi ya Watu ambalo linaweza kuvuruga mfumo mzima wa uchumi huo.
Dr. Ramakrishna alifahamisha kwamba Sekta ya Utalii ambayo kwa sasa
inashikilia nafasi ya Tatu kwa Uchumi wa Dunia ni sehemu kubwa
inayoweza kusukuma kwa haraka Uchumi wa Zanzibar na kubadilisha ustawi
wa Wananchi wake.
Alisema Mchezo wa Golf unaojumuisha na kuchezwa na Watalii wenye
kipato cha juu Duniani una nafasi pana ndani ya Sekta ya Utalii na
akaitolea Mfano Nchi ya Mauritius ilivyokuwa Kiuchumi ndani ya kipindi
kifupi baada ya kuamua kuimarisha Mchezo huo.
Naibu Waziri Mkuu Mstaafu huyo wa Mauritius aliishauri Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia watendaji wakuu hao wa Taasisi za Kiuchumi
na Uwekezaji kuangalia mbinu zitakazowezesha kuanzishwa huduma za
Matibabu na pamoja na ujenzi wa Kumbi za Mikutano ya Kimataifa katika
lengo la kuufanya Utalii wa Zanzibar unakuwa wa Kimataifa.
Akitoa mawazo yake katika Mkutano huo Waziri wa Biashara, Viwanda na
Masoko Zanzibar Balozi Amina Salum Ali alisema utekelezaji wa mipango
katika miradi ya Maendeleo unakuwa wa kusuasua kutokana na ukosefu wa
umakini kwa baadhi ya watendaji wa Taasisi za Umma.
Balozi Amina alisema hali hiyo pia imeleta usumbufu kwa uwajibikaji
wa Watendaji wa Umma kutokana na baadhi ya vikwazo vya Wanasiasa vya
kutowaamini wawekezaji wa sekta Binafsi wanaoamua kutaka kuwekeza miradi
yao Visiwani Zanzibar.
Mapema asubuhi Dr. Ramakrishna Sithanen alikutana kwa mazungumzo na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambapo
walikubaliana hoja ya Zanzibar na Mauritius kubadilishana uzoefu katika
harakati za kuimarisha uchumi wa pande hizo mbili.
Balozi Seif alisema Zanzibar na Mauritius kwa vile ni visiwa
vilivyomo ndani ya Bahari ya Hindi vinastahiki kufanya kazi kwa
kushirikiana hasa katika uanzishwaji wa Viwanda vya kusindika samaki
kutokana na kuzunguukwa na Bahari sehemu zote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Dr. Ramakrishna kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha Sekta
ya Utalii inayotegemewa kuwa muhimili wa uchumi wa Taifa imekusudia
kuongeza nguvu zake katika uzalishaji wa mazao ya viungo ili kuwapa
fursa watalii wanaoingia nchini kufaidika na mazao hayo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/6/2017.
chanzo: zanzibar24.
Comments